Katika tukio la kusikitisha, Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limedungua ndege ya kusafirisha misaada ya kibinadamu katika mkoa wa Kivu Kusini, karibu na eneo la Minembwe. Ndege hiyo ilikuwa ikisafirisha dawa na chakula kwa waathiriwa wa vita vinavyoendelea mashariki mwa DRC.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa, watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo wamepoteza maisha. Misaada yote ya dawa na chakula iliyokuwa ikisafirishwa pia imeharibiwa katika tukio hilo.

Jeshi la DRC, kupitia msemaji wake Generali Sylvain Ekenge, limetoa taarifa rasmi kupitia runinga ya taifa likisema kuwa ndege hiyo ya kiraia haikuwa na kibali cha kupaa katika anga ya DRC, jambo lililosababisha jeshi kuchukua hatua ya kuidungua kwa mujibu wa taratibu za ulinzi wa anga.

Kwa upande mwingine, vuguvugu la waasi wa AFC/M23 limelaani vikali tukio hilo, wakilitaja kama kitendo cha kikatili dhidi ya operesheni za misaada ya kibinadamu. Msemaji wa vuguvugu hilo amesema kuwa shambulizi hilo ni uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa moja kwa moja wa mkataba wa amani uliosainiwa kati ya DRC na Rwanda mjini Washington chini ya saa 72 zilizopita.

AFC/M23 imesema kuwa kuwalenga wafanyakazi wa misaada ni hatua inayorudisha nyuma juhudi za kuleta amani na inaweza kuchochea tena mzozo uliokuwa unaelekea kutatuliwa.

Hadi sasa, mashirika ya misaada ya kibinadamu hayajatoa tamko rasmi kuhusu tukio hili.

Habari hii imeandaliwa na MANGWA

#DRC #KivuKusini #Misaada #Amani #MANGWA