
Walikale – Maafisa Wawili wa AFC/M23 Wakamatwa na Wazalendo
Usiku wa kuamkia Jumatatu, tarehe 1 Julai 2025, wapiganaji wa Wazalendo wamefanikiwa kuwatia mbaroni makamanda wawili wa kundi la waasi wa AFC/M23 katika kijiji cha Misinga, wilayani Walikale, Kivu Kaskazini.
Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani vya eneo hilo, makamanda hao walikamatwa walipokuwa wakisafiri kati ya vijiji vya Kirumburumbu na Muuli. Baada ya kutiwa nguvuni, walipelekwa haraka katika makao makuu ya Wazalendo yaliyoko Buhimba. Hadi sasa, hatma ya maafisa hao bado haijulikani.
Kwa upande wao, wapiganaji wa AFC/M23 walifanya msako mkubwa katika misitu ya eneo hilo lakini hawakufanikiwa kuwapata makamanda wao waliokamatwa. Kwa hasira, waliwalazimisha wakulima wa maeneo jirani kuacha shughuli zao na kushiriki katika msako huo, hali iliyosababisha hofu na machafuko miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Tukio hili linaonyesha wazi kuwa mapigano kati ya Wazalendo na waasi wa AFC/M23 yanaendelea na hali ya usalama katika Walikale bado ni tete, huku raia wakiendelea kubeba mzigo wa vita hivi.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesisitiza kuwa Wazalendo wanaendelea kuwa ngome muhimu ya upinzani dhidi ya vikundi vinavyoungwa mkono na jeshi la Rwanda, hasa kundi la M23-AFC.
Mwandishi:
MANGWA
