Sud-Kivu: Operesheni Kubwa ya Kutambua Wanajeshi wa FARDC na Wazalendo Yaanza

Sud-Kivu | RDC – Serikali ya mkoa wa Sud-Kivu imeanzisha operesheni kubwa ya kutambua wanajeshi wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) pamoja na wapiganaji wa Wazalendo, ikiwa ni hatua ya kulisafisha jeshi na kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Tangazo hilo lilitolewa na Gavana wa Sud-Kivu, Profesa Jean-Jacques Purusi wakati wa maadhimisho ya miaka 65 ya uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mnamo tarehe 30 Juni 2025.

“Kumekuwa na matukio ya usaliti wakati wa kuporomoka kwa baadhi ya maeneo katika Sud-Kivu. Baadhi ya vikosi vilijiondoa kwenye maeneo yao kwa maelezo yasiyoeleweka. Waasi wa M23 hawakuwa na nguvu kuliko sisi,” alisema Gavana Purusi kwa masikitiko, akieleza kuwa mapungufu ya ndani yamechangia mafanikio ya adui.

Operesheni hiyo, inayotarajiwa kuanzia katika mji wa Uvira, inalenga kuwatambua wapiganaji wa kweli na kuwaondoa wale wa kufikirika waliopo kwenye orodha. Itahusisha wanajeshi wa FARDC, wapiganaji wa Volontaires pour la Défense de la Patrie (VDP) pamoja na vikundi vya Wazalendo. Baada ya zoezi la utambuzi, kutakuwa na mchakato wa kupanga upya na kuweka alama za utambulisho kwa vikundi vyote vinavyohusika katika ulinzi wa taifa.

Zaidi ya kuongeza usalama, Gavana Purusi amesema kuwa operesheni hiyo inalenga kuhakikisha usimamizi mzuri wa vifaa na fedha za jeshi.

“Tutahakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya operesheni zinatumika kwa uwazi na askari wetu wanapewa haki zao, wanapata chakula cha kutosha na malazi yanayofaa,” aliongeza.

Kwa mkoa wa Sud-Kivu, hatua hii inaonekana kama mwanzo mpya wa kujenga jeshi imara, lenye uaminifu na linaloaminika na wananchi wake.

Timu maalum kutoka Kinshasa tayari ipo kazini kwa utekelezaji wa mpango huu. Muda wa kurejesha heshima ya jeshi la Congo umeanza rasmi.

✍️ Habari imeandaliwa na MANGWA