
Kinshasa – Juni 14, 2025 – Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imechukua hatua kali dhidi ya aliyekuwa Kamanda wa Kanda ya 33 ya kijeshi katika mkoa wa Kivu Kusini, Jenerali Yav Avul, ambaye sasa amehamishiwa rasmi katika gereza la kijeshi la Ndolo, Kinshasa.
Jenerali huyo anashtakiwa kwa kosa la woga wa kivita na kuikimbia ngome ya kijeshi mbele ya adui, bila kutoa amri ya mapambano wala kusimamia majeshi katika ulinzi wa raia.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi, Jenerali Yav anadaiwa kutelekeza majukumu yake ya uongozi katika hali ya taharuki ya mapigano dhidi ya waasi wa M23/AFC, hali iliyochangia kuporomoka kwa udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Kivu Kusini.
Hatua ya kumkamata na kumfungulia mashitaka ni sehemu ya msimamo mpya wa serikali na jeshi la FARDC kuimarisha nidhamu ya kijeshi, katika harakati za kurejesha heshima na ufanisi wa majeshi ya taifa katika vita vya mashariki mwa nchi.
Kesi ya Jenerali Yav inatarajiwa kusikilizwa na mahakama ya kijeshi ya Kinshasa, huku raia na vyombo vya habari wakifuatilia kwa karibu tukio hili linalozua mjadala kuhusu uwajibikaji wa makamanda wa juu katika vita vinavyoendelea mashariki mwa DRC.
✍🏾 Mwandishi: MANGWA
#SudKivu #FARDC #Ndolo #DRCNews #MANGWA
