
Sean Combs Ajitetea Kwenye Kesi ya Uhalifu wa Kijinsia: Wakili Wake Asema Ni Mahusiano Ya Watu Wazima Walioridhiana
New York — Msanii na mfanyabiashara maarufu Sean Combs, anayefahamika pia kama Diddy, ameendelea kujitetea mbele ya mahakama ya shirikisho jijini Manhattan, huku akikabiliwa na mashitaka mazito ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ukahaba, uhalifu wa kihalifu (racketeering), na kula njama ya kuendeleza biashara hiyo.
Kwa zaidi ya wiki sita, mahakama hiyo imesikiliza ushahidi wa mashahidi zaidi ya ishirini na tano, wakiwemo wake wa zamani, wafanyakazi wa zamani, na maafisa wa sheria. Serikali ya Marekani inamtuhumu Combs kwa kuendesha mtandao wa kihalifu uliokuwa unaficha na kuwezesha vitendo vya udhalilishaji kwa miongo kadhaa. Combs amekana mashtaka yote.
Combs Atuhumiwa Kupiga na Kulazimisha Wakina Mama
Ushahidi mkubwa katika kesi hii umejikita kwenye video ya usalama wa hoteli iliyomwonyesha Combs akimshambulia mpenzi wake wa zamani, Cassie Ventura, mwaka 2016. Ventura ameshuhudia kuwa Combs alikuwa akimshambulia mara kwa mara, kumlazimisha kushiriki vitendo vya kingono na wanaume wengine huku Combs akitazama na kuongoza.
Lakini mawakili wa Combs wamekiri kwamba mteja wao ana historia ya ukatili wa majumbani, lakini wamesisitiza kuwa hakuna mtu aliyelazimishwa kufanya mapenzi kwa nguvu. Wameeleza kuwa mahusiano hayo yalikuwa ya hiari, japo yalikuwa na wivu na migogoro.
Uhusiano wa Kipekee Au Utumwa wa Kisasa?
Mawakili wa Combs wameeleza kuwa maisha yake ya kingono yalikuwa ya “mtindo wa kipekee” na kwamba Cassie Ventura pamoja na mwanamke mwingine aliyejitambulisha kama “Jane” walikubali kushiriki katika mahusiano hayo ya watu wengi kwa hiari yao.
Kulingana na mawakili wa utetezi, wanawake hao walitaka kumfurahisha Combs ili kuimarisha mahusiano yao naye. Ushahidi wa video uliooneshwa mahakamani ulionesha matukio ya kingono baina ya Combs, Ventura, na watu wengine, lakini mawakili wa Combs wamesema video hizo zinaonesha mahusiano ya ridhaa, siyo udhalilishaji.
Utetezi: Ni Vita ya Pesa
Mawakili wa Combs pia wamedai kuwa mlolongo wa mashitaka dhidi ya mteja wao ni jaribio la watu kutafuta fedha kwa kupitia jina lake kubwa. Tangu Cassie Ventura afungue kesi ya madai ya kiraia dhidi ya Combs mwezi Novemba 2023, zaidi ya watu wengine wamejitokeza na madai kama hayo.
Combs amekuwa akikanusha madai yote, huku mawakili wake wakisisitiza kuwa hakuna mtandao wa kihalifu na kwamba maisha yake ya binafsi hayawezi kuchanganywa na maisha yake ya kazi. Wafanyakazi wake wa zamani wameeleza mahakamani kuwa walihusika kununua dawa za kulevya na kuandaa vyumba vya hoteli, lakini waliona hayo ni sehemu ya maisha binafsi ya Combs.
Hatua Inayofuata
Kesi hii, ambayo imevutia macho ya dunia nzima, inaelekea ukingoni huku upande wa utetezi ukitarajia kutumia muda mfupi sana kujitetea. Inaonekana Combs hatapanda kizimbani kujitetea moja kwa moja.
Iwapo mahakama itampata Combs na hatia ya mashtaka haya mazito, anaweza kukabiliwa na kifungo cha muda mrefu gerezani.
Habari hii imeandaliwa na MANGWA
#SeanCombs #Mahakama #SexTrafficking #NewYork #MANGWA
