
🇨🇩📰 HABARI MPYA: Ripoti ya Umoja wa Mataifa Yafichua Ushirikiano Mpya wa Rwanda na Waasi wa M23 Mashariki mwa DRC
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imezua taharuki kubwa katika uhusiano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda. Kulingana na nyaraka za siri zilizotolewa na kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa na kuripotiwa na shirika la habari la Reuters, Rwanda inadaiwa kuendelea kuisaidia kijeshi kundi la waasi wa M23, licha ya makubaliano ya amani yaliyosainiwa tarehe 27 Juni 2025 mjini Washington.
Kulingana na ripoti hiyo:
🔸 Serikali ya Rais Paul Kagame inadaiwa kutoa mafunzo kwa wapiganaji wapya wa M23 na kuwapa silaha za hali ya juu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya teknolojia vinavyoweza kushambulia ndege za jeshi la FARDC.
🔸 Rwanda inakanusha madai hayo, ikisisitiza kuwa hatua zake Mashariki mwa Congo ni za kujihami dhidi ya vitisho vya kundi la FDLR, ambalo linahusishwa na wahusika wa mauaji ya halaiki ya 1994.
🔸 Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa malengo ya Rwanda hayahusiani tena na kupambana na FDLR pekee, bali ni mpango mpana wa kudhibiti maeneo muhimu katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini.
🔸 Takriban wanajeshi 6,000 wa Rwanda wanadaiwa kuwa ndani ya ardhi ya DRC, huku wengine zaidi wakiwa kwenye mpaka wakiwa tayari kuingilia mapambano.
Katika kipindi hiki cha hatari:
Ripoti hii inakuja siku chache tu baada ya kusainiwa kwa mkataba wa amani kati ya DRC na Rwanda kwa usimamizi wa Marekani. Rais Donald Trump, aliyesimamia moja kwa moja mazungumzo hayo, ametishia vikwazo vikubwa kwa upande wowote utakaokiuka makubaliano hayo.
Serikali ya Congo bado haijatoa tamko rasmi kuhusiana na ripoti hii mpya.
Habari hii imeandikwa na:
✍️ MANGWA
