🇨🇩 

RDC Yasitisha Mpango wa Kuondoka kwa MONUSCO Kufuatia Kuzorota kwa Usalama Mashariki

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC) imetangaza kuwa mpango wa kuondoka kwa Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha MONUSCO hauwezi kuendelea kwa sasa kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na kibinadamu katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Hippolyte Mfulu Kingonzila, Mshauri Mkuu na Kaimu Balozi wa Kudumu wa RDC katika Umoja wa Mataifa, alifafanua kuwa mpango huo ulikuwa umepangwa kuwasilishwa ifikapo Machi 31, 2024, lakini ulisitishwa rasmi kutokana na ongezeko la machafuko tangu Januari 2025.

“Mpango wa mkakati wa kuondoka kwa MONUSCO kwa hatua, kwa uwajibikaji na kwa njia endelevu, umeahirishwa kwa sasa. Serikali itaurejesha mezani wakati hali ya usalama itakapokuwa imetengemaa,” alisema Hippolyte Mfulu.

Katika taarifa hiyo, serikali ya Congo imetoa wito kwa Baraza la Usalama kuongeza mamlaka na uwezo wa MONUSCO ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo katika mazingira ya sasa yenye changamoto kubwa.

Aidha, Kingonzila aliishukuru Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na askari wake kwa msaada walioutoa katika kipindi kigumu cha historia ya Congo. Alibainisha kuwa uamuzi wa kuondoa kikosi cha SADC (SAMIDRC) uliopitishwa Machi 13, 2025 na wakuu wa nchi za SADC, ulimaliza rasmi jukumu la msaada wa kimkakati na vifaa uliokuwa ukitolewa na MONUSCO kupitia azimio la Umoja wa Mataifa la Agosti 2024.

Kwa upande mwingine, ingawa MONUSCO ilifunga ofisi yake ya Bukavu tarehe 25 Juni 2024 kama sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango wa kujiondoa, hali ya usalama inazidi kuwa mbaya hasa baada ya waasi wa M23 kuendelea kudhibiti maeneo makubwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Ikumbukwe kuwa mnamo Desemba 2024, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilirefusha rasmi muda wa MONUSCO hadi Desemba 20, 2025, licha ya hatua ya awali ya kuanza kujiondoa.

Kwa sasa, serikali ya Marekani kupitia ujumbe wake katika Umoja wa Mataifa imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuipatia MONUSCO mamlaka na rasilimali za kutosha ili kusaidia utekelezaji wa mkataba wa amani kati ya Rwanda na Congo uliotiwa saini mjini Washington.

📝 Mwandishi: MANGWA