Kinshasa, 13 Juni 2025 – Katika kikao cha kawaida cha Ijumaa hii, Senati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilipitisha kwa kauli moja miswada miwili muhimu: mabadiliko ya sheria kuhusu kupambana na utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi, pamoja na mswada wa bajeti ya marekebisho kwa mwaka wa fedha 2025.

Rais wa Senati, Jean-Michel Sama Lukonde, alitangaza matokeo ya upigaji kura kwa sauti ya furaha:

“Kati ya maseneta 109, ni 78 waliohudhuria na wote 78 walipiga kura ya ndiyo. Hakuna aliyepiga kura ya hapana wala kujizuia. Matokeo haya ni sawa kwa miswada yote miwili.”

Mswada wa kwanza unalenga kuboresha sheria kuhusu kupambana na utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi pamoja na uenezaji wa silaha za maangamizi ya halaiki, huku mswada wa pili ukiwa ni bajeti ya marekebisho kwa mwaka 2025, ikijumuisha mabadiliko ya kiuchumi na kipato cha taifa.

Kwa kuwa kulikuwa na tofauti katika baadhi ya vipengele kati ya Bunge na Senati, kamati ya pamoja ya masuala ya kiuchumi na fedha kutoka pande zote mbili itaandaliwa kwa ajili ya kufanikisha maridhiano ya vipengele vilivyopingwa hususan katika mswada wa kwanza kuhusu utakatishaji wa fedha.

Hatua hii ya Senati inachukuliwa kama hatua muhimu kuelekea kuimarisha usalama wa kifedha wa taifa, kuongeza uwajibikaji, na kuonyesha dhamira ya DRC kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kupambana na mitandao ya kifedha haramu.

✍🏾 Mwandishi: MANGWA

#SenatiDRC #UtakatishajiWaFedha #Bajeti2025 #MANGWA

By mangwa