RAIS RAMAPHOSA AMWEKA PEMBENI WAZIRI WA POLISI MCHUNU KUFUATIA TUHUMA NZITO ZA RUSHWA NA USHIRIKIANO NA MAGENGO YA UJAMBAZI

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI | Reuters — Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ametangaza kumpumzisha mara moja Waziri wa Polisi Senzo Mchunu kutoka majukumu yake, kufuatia tuhuma nzito zilizoibuliwa na Kamishna wa Polisi wa jimbo la KwaZulu-Natal, Nhlanhla Mkhwanazi, kwamba Mchunu alishirikiana na mtandao wa kihalifu na akaingilia uchunguzi wa kesi kubwa zinazohusiana na mauaji ya kisiasa.

Katika taarifa rasmi aliyoitoa kwa umma kupitia vyombo vya habari vya serikali na binafsi, Ramaphosa alieleza kuwa tuhuma hizi ni za kiwango cha juu cha uzito, na kwamba zimetikisa imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa haki na usalama wa taifa.

“Tuhuma hizi zinahitaji uchunguzi wa haraka na wa kina. Hii siyo jambo la kawaida – ni tishio kwa utawala wa sheria na haki,” alisema Rais Ramaphosa. “Nitaanzisha tume maalum ya kimahakama kuchunguza jambo hili kwa kina.”

Kwa mujibu wa Ramaphosa, Profesa wa Sheria Firoz Cachalia ameapishwa kama kaimu waziri wa polisi hadi uchunguzi utakapo kamilika.

Mchunu Akana Tuhuma, Asema Ni Za Kisiasa

Waziri Mchunu, ambaye pia ni mwanachama mwandamizi ndani ya Chama cha ANC, alikanusha vikali tuhuma hizo wiki iliyopita, akisema hazina msingi wowote. Kupitia msemaji wake, alisisitiza kuwa anaendelea kuwa mtu wa kuheshimu sheria na yuko tayari kushirikiana na uchunguzi wowote.

Lakini kile kilichowasha moto ni mkutano wa waandishi wa habari wa Kamishna Mkhwanazi, ambapo alieleza kuwa Mchunu alihusika kuvunja kikosi maalum cha uchunguzi wa mauaji ya kisiasa, kwa lengo la kulinda wanasiasa, maafisa wa polisi, na watu wengine waliotajwa kuhusika na magenge ya uhalifu ya kisiasa.

Mkhwanazi alifichua kuwa zaidi ya jalada 100 za kesi zilitolewa kutoka kwa kikosi hicho na hakuna hata moja lililochunguzwa tena tangu wakati huo.

Aidha, Kamishna huyo alisema ana ushahidi wa kidijitali unaojumuisha ujumbe wa WhatsApp unaodaiwa kumhusisha Mchunu moja kwa moja na maamuzi ya kuvunja kikosi hicho.

ANC, Vyama Vingine vya Siasa, na Wawekezaji Wapaza Sauti

Wachambuzi wa siasa wanasema Senzo Mchunu alikuwa mgombea anayeonekana kuwa na nafasi ya kugombea uongozi mkuu wa ANC mwaka 2027, hivyo kashfa hii ina athari kubwa kisiasa.

Chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), ambacho ni mshirika mkuu wa ANC katika serikali ya mseto, kimetaka uchunguzi wa bunge kufanyika mara moja juu ya tuhuma dhidi ya Mchunu. Vyama vingine vya upinzani navyo vimesema Mchunu asimamishwe kazi rasmi na si tu kupumzishwa.

Kwa upande mwingine, wawekezaji wa ndani na wa kimataifa wamekuwa wakilalamikia hali ya uhalifu nchini Afrika Kusini kwa muda mrefu. Benki ya Dunia (World Bank) imekadiria kuwa uhalifu huo unagharimu taifa hilo hadi asilimia 10 ya pato la taifa (GDP) kila mwaka.

Tuhuma dhidi ya waziri wa polisi ni pigo kubwa kwa juhudi za Rais Ramaphosa ambaye alikuja madarakani kwa ahadi ya kupambana na rushwa, kulinda taasisi za sheria, na kurejesha imani ya umma katika serikali.

✍🏽 Imeandikwa na: MANGWA