Rais Tshisekedi Azindua Forum ya Kitaifa ya Haki ya Fidia kwa Waathirika wa Unyanyasaji wa Kijinsia na Uhalifu wa Kibinadamu

Kinshasa — Jumanne hii, katika Kituo cha Kitamaduni na Kisanii cha Nchi za Afrika ya Kati (CCAPAC), Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo, akiwa ameandamana na Mkewe, Mama wa Taifa Denise Nyakeru Tshisekedi, ameongoza uzinduzi rasmi wa Forum ya Kitaifa kuhusu Haki ya Fidia.

Tukio hili limeandaliwa na FONAREV (Mfuko wa Kitaifa wa Fidia kwa Waathirika wa Unyanyasaji wa Kijinsia unaohusiana na Migogoro na Waathirika wa Uhalifu dhidi ya Amani na Usalama wa Binadamu), kwa kushirikiana na Wizara ya Haki za Binadamu, na linatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 1 hadi Julai 4, 2025, jijini Kinshasa.

Rais: “Hii si Mkutano wa Kawaida”

Katika hotuba yake, Rais Tshisekedi alieleza kuwa Forum hii ni hatua ya kihistoria inayovunja ukimya na kutojali wa miaka mingi.

“Mkutano huu haupaswi kuchukuliwa kama tukio la kawaida. Hii ni ishara ya taifa lililoamua kuweka heshima na haki kwa waathirika kuwa kiini cha safari yake ya maridhiano na ujenzi wa taifa jipya,” alisema Rais.

Akiweka mkazo juu ya athari za Genocost (Mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Congo kwa faida za kiuchumi), Rais Tshisekedi alisisitiza kuwa:

“Congo haiwezi kujijenga juu ya majeraha yaliyopuuzwa. Fidia si upendeleo, bali ni haki. Tunawadaiwa waathirika hawa ukweli, haki, fidia, na mustakabali mpya wa amani na utu,” aliongeza.

Serikali Yasisitiza Utekelezaji wa Haki

Rais Tshisekedi alitumia fursa hiyo kurudia ahadi yake ya kujenga mazingira bora kwa waathirika, hasa baada ya kutiwa saini kwa Makubaliano ya Amani ya Washington yaliyolenga kumaliza mzozo wa muda mrefu mashariki mwa nchi.

“Hatuwezi kuwasaliti waathirika. Tunawawajibikia leo, kesho na milele kuhakikisha kwamba vitendo hivi vya kikatili havitarudi tena,” alisema Rais.

FONAREV: “Fidia ni Zaidi ya Malipo ya Fedha”

Mkurugenzi Mkuu wa FONAREV, Bw. Patrick Fata, alieleza kuwa:

“Fidia haiishii kwenye malipo ya kifedha pekee. Ni hatua ya kutambua, kuponya jamii zilizovunjika, na kurejesha heshima ya waathirika.”

Naye Waziri wa Haki za Binadamu, Bi. Chambu Mwavita, alisema:

“Fidia ni haki halali, ni msingi wa amani ya kudumu, na ni ujumbe wenye nguvu kwa waathirika kuwa hawajasahaulika.”

Hatua ya Kihistoria kwa Taifa

Forum hii inalenga kukamilisha mkakati wa kitaifa wa fidia na kuzindua rasmi mipango ya utekelezaji wa haki hiyo.

Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi wa serikali, wanadiplomasia, asasi za kiraia na wawakilishi wa waathirika, ikiwa ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za kitaifa za kukumbuka na kuponya majeraha ya kihistoria ya Congo.

Habari hii imeandaliwa na MANGWA

#FidyaRDC #ForumKinshasa #FONAREV #HakiKwaWaathirika #MANGWA