
Marekani Yafunga Rasmi USAID, Yatangaza Dira Mpya ya Misaada ya Kigeni
Jumanne, Julai 1, 2025, Marekani imetangaza rasmi kusitisha shughuli zote za Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID) katika msaada wa maendeleo ya kigeni. Uamuzi huu umetangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambaye alieleza kuwa huu ni mwanzo wa enzi mpya ya ushirikiano wa kimataifa unaoweka mbele maslahi ya taifa la Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kuanzia sasa misaada yote ya kigeni itasimamiwa moja kwa moja na wizara hiyo kwa lengo la kuhakikisha kwamba msaada wowote wa Marekani unaleta faida ya moja kwa moja kwa taifa hilo.
USAID Yalaumiwa kwa Kutokufanikisha Malengo
Wizara hiyo ilieleza kuwa uchunguzi wa kina uliofanywa na utawala wa Rais Donald Trump ulibaini kuwa USAID imeshindwa kufikia malengo yake licha ya kutumia mabilioni ya dola kwa miongo kadhaa. “USAID imeshindwa kuongeza ushawishi wa Marekani, kukuza maendeleo ya kiuchumi duniani, na imechangia zaidi kuundwa kwa mtandao mkubwa wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) ambayo yamekuwa mzigo kwa walipa kodi wa Marekani,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Wizara iliongeza kuwa misaada hiyo mara nyingi haikuleta mabadiliko yaliyokusudiwa na badala yake ilichochea chuki dhidi ya Marekani katika mataifa mengi ya walengwa, hasa katika Afrika na Mashariki ya Kati.
Marekani Yaweka Kipaumbele kwa Maslahi Yake
Kwa utawala wa Trump, misaada ya sasa itakuwa na vigezo vya kuchagua mataifa yatakayofaidika, kipaumbele kikitolewa kwa mataifa yanayoonyesha uwezo wa kujitegemea na yaliyo tayari kushirikiana kwa dhati na Marekani. Misaada hiyo itaelekezwa zaidi katika kuimarisha sekta binafsi na kukuza uwekezaji, hasa kwa kampuni za Marekani.
Aidha, Marekani itaweka alama ya bendera yake kwenye misaada yote ili wananchi wa mataifa yanayonufaika wafahamu moja kwa moja kuwa misaada hiyo inatoka kwa watu wa Marekani na si mashirika yasiyo ya kiserikali yasiyojulikana.
Athari Zaanza Kujitokeza DRC
Tangu kutangazwa kwa kusitishwa kwa misaada hiyo mwezi Januari, Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ameshaelekeza serikali yake kuchukua hatua za haraka kushughulikia pengo la fedha lililosababishwa na uamuzi huo.
Rais Tshisekedi ameonya kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa huduma za msingi kama vile afya, elimu, kilimo, na usafi wa mazingira, na inaweza kuzidisha mgogoro wa kibinadamu katika maeneo mbalimbali, hasa mashariki mwa DRC.
Tayari Marekani imefuta mpango muhimu wa usambazaji wa vifaa vya dharura kwa waathiriwa wa vita mashariki mwa DRC. Vifaa hivyo vilijumuisha dawa za kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU), magonjwa ya zinaa, na mimba zisizotarajiwa.
Hatua Mpya ya Marekani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeeleza kuwa misaada ya sasa itaelekezwa kwa mataifa yanayothamini biashara badala ya misaada ya moja kwa moja. “Tunataka kuwekeza, sio kusaidia. Tunataka kujenga ushirikiano wa kweli unaozingatia maslahi ya Marekani,” alisema msemaji wa wizara hiyo.
Mpango huu mpya pia unalenga kukabiliana na ushawishi wa China katika bara la Afrika na kanda nyingine duniani kwa kuhamasisha ushirikiano wa kibiashara unaotanguliza maslahi ya Marekani.
Mataifa Yanapewa Onyo
Mataifa yanayopokea msaada wa Marekani yanatakiwa kuelewa kuwa misaada hiyo haitakuwa ya kudumu. Marekani itawekeza tu kwenye miradi yenye tija, yenye uwazi, na yenye faida ya haraka kwa pande zote mbili.
Tunaendelea kufuatilia hali hii na athari zake kwa mataifa yanayoitegemea Marekani katika miradi ya maendeleo.
✍🏽 MANGWA
