Kombora la Sajil la Iran: Silaha Hatari Katika Mzozo wa Hivi Karibuni na Israel

Katika mvutano wa kijeshi uliotokea kati ya Israel na Iran wiki zilizopita, kombora la Sajil-2 la Iran limekuwa moja ya mada kuu za mjadala na tahadhari ya kimataifa. Iran ilithibitisha kwa mara ya kwanza kuwa ililitumia kombora hilo katika mashambulizi dhidi ya Israel, likiwa sehemu ya “Operesheni Ahadi ya Kweli 3.”

Walinda Mapinduzi wa Iran walisema kuwa mashambulizi hayo yalikuwa ni kulipiza kisasi dhidi ya Israel, wakieleza kuwa kombora la Sajil ni miongoni mwa silaha zao zenye nguvu zaidi, likiwa na uwezo mkubwa wa uharibifu na usahihi wa hali ya juu.

Nguvu ya Kombora la Sajil

Kombora la Sajil lina uwezo wa kufika umbali wa hadi kilomita 2,000, jambo linalowezesha Iran kulenga maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati, kusini mashariki mwa Ulaya, na sehemu za Asia ya Kati. Kwa mfano, likirushwa kutoka mji wa Natanz, linaweza kufika Tel Aviv, Israel ndani ya dakika saba pekee.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Walinda Mapinduzi wa Iran, Sajil ni kombora la hatua mbili linalotumia mafuta yaliyo tayari kwa matumizi (solid fuel), jambo linaloliwezesha kuzinduliwa haraka bila maandalizi ya muda mrefu. Iran inadai kuwa kombora hili linaweza kulenga vituo vya kijeshi, miji mikubwa, na maeneo yenye miundombinu nyeti.

Israel Yadai Kulinasua

Jeshi la Israel lilitangaza kuwa mfumo wake wa ulinzi wa anga uliweza kulinasua kombora la Sajil na kuzuia athari yoyote kubwa. Israel ilisema kuwa licha ya mashambulizi ya Iran, mifumo yake ya ulinzi kama Iron Dome na David’s Sling ilifanya kazi kwa ufanisi mkubwa kuzuia hatari hiyo.

Umuhimu wa Sajil Katika Ushindani wa Kijeshi

Wachambuzi wa kijeshi wanaamini kuwa Sajil ni moja ya silaha zinazoongeza tishio la Iran katika Mashariki ya Kati. Uwezo wake wa kushambulia kwa umbali mrefu na kwa kasi kubwa umeiweka Israel na washirika wake katika hali ya uangalizi mkali.

Licha ya kusitishwa kwa mapigano hivi karibuni, uwepo wa silaha kama Sajil unazidi kuifanya hali ya usalama katika kanda hiyo kuwa tete. Marekani na washirika wake wameonya kuwa mzozo huo unaweza kurudiwa kwa urahisi ikiwa hatua za kudumu za kidiplomasia hazitachukuliwa.

Kwa sasa, dunia inasubiri kuona ikiwa makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano yataweza kudumu, huku kombora la Sajil likisalia kuwa silaha inayotajwa kama tishio kubwa la kiistratejia katika eneo hilo.

Habari hii imeandaliwa na MANGWA