
KENYA: Idadi ya Waliopoteza Maisha Katika Maandamano Yaongezeka Hadi 16
Idadi ya raia waliopoteza maisha kufuatia maandamano ya Jumatano nchini Kenya imefikia watu 16. Shirika la kimataifa la haki za binadamu, Amnesty International, limethibitisha takwimu hizo, likieleza kuwa wengi wa waathirika walifariki kutokana na majeraha ya risasi.
Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International, Irungu Houghton, alisema kuwa idadi hiyo imethibitishwa na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya, ambayo imekuwa ikifuatilia kwa karibu matukio ya maandamano hayo.
Maandamano hayo yalifanyika kwa lengo la kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano makubwa ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024, ambayo mwaka jana yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 60 na kujeruhi mamia wengine.
Katika maandamano ya Jumatano, polisi walifunga barabara kuu zinazoelekea katikati ya jiji la Nairobi, huku majengo ya serikali yakizingirwa kwa ulinzi mkali. Waandamanaji wengi, hususan vijana, walikusanyika wakiwa na mabango na bendera za taifa la Kenya, wakipaza sauti zao kudai haki na kutetea wale waliopoteza maisha mwaka jana.
“Ni muhimu kwamba vijana wa Kenya waendelee kuadhimisha siku hii, wakikumbuka wale waliopoteza maisha yao katika harakati hizi,” alisema Angel Mbuthia, mmoja wa viongozi wa vijana.
Taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya maandamano na hatua zinazochukuliwa na serikali zitaendelea kutolewa kadri hali inavyoendelea.
Muandishi: MANGWA
#Kenya #Maandamano #HakiZaBinadamu #HabariZaAfrika #MCMR
