
Iran imepanga kukutana na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani mjini Istanbul siku ya Ijumaa kujadili mzozo wa mpango wake wa nyuklia, huku ikitupia lawama mataifa ya Ulaya kwa kuvuruga mkataba wa kihistoria wa nyuklia wa mwaka 2015. Hii ni mara ya kwanza kwa pande hizo kukutana tangu vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel mwezi uliopita, ambavyo vilisababisha Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya vinu vya nyuklia vya Tehran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alithibitisha kuwa urutubishaji wa uranium umesimama kwa sasa kutokana na uharibifu mkubwa, lakini akaweka wazi kuwa taifa hilo “haliwezi kuachana na urutubishaji kwani ni fahari ya kitaifa”.
Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kupitia Truth Social kuwa Marekani “itashambulia tena ikiwa itahitajika”.
Mkataba wa mwaka 2015, uliohusisha mataifa sita yenye nguvu duniani, ulilenga kuzuia Iran kuendeleza silaha za nyuklia kwa kuruhusu ukaguzi na kuweka viwango vya chini vya urutubishaji. Hata hivyo, Marekani ilijiondoa kwenye mkataba huo mwaka 2018 chini ya Trump, na kurejesha vikwazo vikali.
Tangu hapo, Iran imeanza kupuuza baadhi ya masharti ya mkataba huo huku ikilalamikia kutotekelezwa kwa ahadi za Ulaya. Mataifa ya Ulaya sasa yanatishia kurejesha vikwazo kupitia kifungu cha “snapback” ikiwa hakuna suluhisho litakalofikiwa kufikia mwisho wa Agosti.
Wakati huo huo, Iran imefanya mkutano wa pande tatu na China na Urusi kuhusu suala hilo, huku Beijing ikiahidi kuendeleza juhudi za kurudisha mazungumzo ya amani.
Wakati Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) likiripoti kuwa Iran ndiyo nchi pekee isiyo na silaha za nyuklia inayorutubisha uranium kwa asilimia 60, hatua inayozua hofu ya matumizi ya kijeshi, Iran inasisitiza mpango wake ni kwa matumizi ya kiraia tu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesema Tehran haina mpango wowote wa kuzungumza na Marekani kwa sasa, akitaja kuwa hatua zake zote zinatekelezwa kwa mujibu wa masharti ya mkataba huo wenyewe.
Kwa sasa, dunia inasubiri kuona kama juhudi hizi mpya za Istanbul zitaleta suluhisho la kidiplomasia kabla mkataba wa awali kumalizika mwezi Oktoba.
MWANDISHI: MANGWA
