Geita: Kijana Auawa Kikatili na Viongozi wa Serikali kwa Tuhuma za Wizi wa Uongo

Familia ya Enock Thomas Mhangwa (25), mkazi wa Runzewe, Geita, imebubujikwa na majonzi kufuatia mauaji ya kikatili aliyofanyiwa kijana wao na viongozi wa serikali wa kijiji. Enock anadaiwa kupigwa hadi kufa na Afisa Mtendaji wa kijiji cha Uyovu aitwaye Budimu na Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lyobahika aitwaye Masembo.

Kwa mujibu wa familia ya marehemu, Enock alituhumiwa kwa wizi wa kompyuta na mashine za kunyolea bila ushahidi wowote. Viongozi hao walimkamata na kumfungia katika ofisi ya kijiji, ambako walimtesa na kumpiga kwa nguvu wakitaka akiri kuhusika na wizi huo. Enock alikana kuhusika na aliomba haki itendeke, lakini walizidi kumtesa.

Baadaye walimchukua hadi nyumbani kwao na kumtaka mama yake awape shilingi laki mbili ili waachane naye. Mama yao alieleza kuwa hakuwa na fedha hizo. Viongozi hao walimwambia mama: “Kama huna laki mbili, huyu tunaenda kummaliza.” Walimchukua Enock hadi porini, wakamfunga mikono nyuma na kuendelea kumpiga bila huruma.

Mashuhuda wanasema Enock alipigwa kwa ukatili hadi walipomvunja mbavu na kumpasua bandama, hali iliyosababisha damu kuvujia ndani. Enock aliwaomba waache, akiahidi kuuza pumba ili kuwalipa pesa walizotaka, lakini walikataa kumsikiliza. Waliendelea kumpiga hadi walipojiridhisha kuwa amefariki ndipo walipomtelekeza na kutoroka.

Baada ya tukio hilo, uchunguzi wa polisi umebaini kuwa vifaa vilivyoibiwa vilikutwa katika saluni ya dada mmoja ambaye alikiri kuvinunua kutoka kwa vijana wawili wasiomhusu Enock. Vijana hao waliokamatwa pia wamethibitisha kwamba hawamjui Enock na hawakushirikiana naye katika wizi wowote.

Familia ya Enock imeeleza kusikitishwa na kitendo hicho cha kinyama, hasa kwa kuwa Enock hakuwa na historia yoyote ya wizi. Mama mzazi wa Enock anaendelea kupata mshtuko mkubwa akijilaumu kwamba kama angekuwa na uwezo wa kutoa pesa waliyoitaka, huenda mwanawe angekuwa hai.

Familia inaomba jamii, viongozi wa haki za binadamu, vyombo vya habari na mamlaka husika kusimama pamoja nao kuhakikisha kwamba waliomtesa na kumuua Enock wanakamatwa haraka na kufikishwa mahakamani ili haki ipatikane.

Kwa sasa, viongozi hao wanaodaiwa kuhusika wanatafutwa na jeshi la polisi.

Imeandikwa na MANGWA