Maelfu ya Wanajeshi wa FARDC Wawasili Kalemie Kwa Ajili ya Kupambana na M23

Kalemie, Tanganyika — Zaidi ya wanajeshi 7,000 wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) na washirika wao wamewasili katika mji wa Kalemie, mkoa wa Tanganyika, kama sehemu ya operesheni kubwa ya kijeshi inayolenga kuimarisha udhibiti wa maeneo yenye machafuko mashariki mwa nchi.

Soma zaidi: Angalia taarifa rasmi ya TV5 Monde

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo TV5 Monde, zinaeleza kuwa kikosi hicho kinajiandaa kwa hatua ya pili ya oparesheni maalum itakayojikita kwenye maeneo ya Uvira na Fizi katika mkoa wa Kivu Kusini, ambako hali ya usalama imeendelea kuzorota kutokana na vitendo vya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na jeshi la Rwanda, kwa mujibu wa serikali ya Kinshasa.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya usalama, huenda lengo kuu la jeshi la FARDC ni kuandaa mashambulizi ya kurejesha miji ya Bukavu na Goma, ambayo kwa sasa imo hatarini kuanguka mikononi mwa waasi au tayari imezingirwa kwa sehemu.

Wakati huo huo, taarifa kutoka TV5 Monde zinaonyesha kuwa waasi wa M23/AFC wameongeza nguvu katika maeneo ya Goma na Bukavu kwa kupeleka wapiganaji wapya, jambo linalotafsiriwa kuwa ni ishara ya kupanua ushawishi wao kuelekea Kivu Kusini.

Katika hali hii ya sintofahamu ya kijeshi, juhudi za kidiplomasia bado hazijazaa matunda. Mkataba wa amani uliotiwa saini hivi karibuni kati ya Rwanda na DRC chini ya usimamizi wa Marekani na washirika wa kimataifa unaendelea kuibua mijadala na sintofahamu nchini, hasa kutokana na kuendelea kwa mapigano.

Wakazi wa maeneo ya mapigano wameachwa katika hofu na mateso, huku visa vya unyakuzi, ubakaji, na wizi vikiongezeka. Maelfu ya raia wameyakimbia makazi yao na kuomba msaada wa haraka kutoka kwa taasisi za misaada ya kibinadamu.

Mwandishi: MANGWA