DRC Yaitaka Uganda Kufafanua Sababu ya Kufungua Mpaka wa Bunagana Bila Ushirikiano Rasmi

MAELEZO KAMILI:

Kinshasa, Julai 2025 – Kufuatia kikao cha Baraza la Mawaziri, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, imeitaka serikali ya Uganda kutoa maelezo ya kina kuhusu uamuzi wa kufungua tena mpaka wa Bunagana wiki hii bila kuwepo kwa maafisa wa serikali ya Congo katika eneo hilo nyeti.

Mpaka wa Bunagana, ambao ni lango muhimu la biashara kati ya DRC na Uganda, ulifunguliwa tena siku ya Alhamisi kwa uamuzi wa upande wa Uganda pekee, huku ripoti zikieleza kuwa hatua hiyo ilitokana na maagizo ya Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kufuatia maelekezo kutoka kwa Rais Yoweri Museveni.

Eneo la Bunagana limekuwa chini ya udhibiti wa waasi wa M23 tangu Juni 2022, jambo lililosababisha mpaka huo kufungwa kwa muda mrefu kwa sababu za kiusalama. Hata hivyo, hatua ya Uganda kufungua mpaka huo bila ushirikiano wa pande zote mbili imezua maswali mazito kuhusu heshima ya mipaka ya kimataifa na usalama wa kitaifa wa DRC.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Congo imeeleza kuwa hatua hiyo ni ya kushangaza na inahitaji majibu ya haraka, kwani haikufuata misingi ya mawasiliano ya kidiplomasia kati ya mataifa yanayoheshimiana.

Aidha, wenyeji wa Bunagana kutoka pande zote mbili wamekuwa wakikumbwa na hali ngumu ya kiuchumi tangu kufungwa kwa mpaka huo, huku ukosefu wa ajira na biashara ukisababisha umasikini mkubwa kwa wananchi wa kawaida. Hali hiyo imewafanya baadhi ya viongozi wa kijamii kuunga mkono kufunguliwa kwa mpaka huo, lakini kwa masharti ya kuwepo kwa usalama na ushirikiano wa pande zote mbili.

Serikali ya DRC imesisitiza kuwa haitakubali hatua zozote zinazokiuka mamlaka yake ya kitaifa na itachukua hatua zinazofaa kulinda heshima na usalama wa raia wake.

MWANDISHI: MANGWA