Dola Milioni 7 Kutoka Congo Zachukuliwa Uwanja wa Ndege Beirut, Lebanon

Mamlaka za Lebanon zimeripoti kukamata kiasi cha dola milioni 7 taslimu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beirut siku ya Jumapili, tarehe 29 Juni. Taarifa hiyo imethibitishwa na L’Orient-Le Jour pamoja na afisa wa juu wa forodha wa Lebanon.

Fedha hizo zilikuwa zimefichwa kwenye mizigo kadhaa ya abiria waliokuwa kwenye ndege kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC). Watu watatu waliokuwa kwenye ndege hiyo wanashukiwa kuhusika katika jaribio hili la kusafirisha fedha kwa njia isiyo halali.

Kwa mujibu wa taarifa, mmoja kati ya watuhumiwa hao alitokea moja kwa moja kutoka Congo, huku wawili wengine wakitoka kwenye nchi nyingine ya Afrika ambayo haijatajwa, lakini walikuwa katika safari ya transit kuelekea Lebanon.

Inaelezwa kuwa washukiwa hao walijaribu kuficha fedha hizo kwa makusudi na walitoa taarifa za uongo kwa maafisa wa forodha wakati wa ukaguzi wa mizigo yao.

Watu hao watatu wamekabidhiwa kwenye kitengo cha makosa ya fedha ili kufanyiwa uchunguzi wa kina. Vyombo vya habari vya Lebanon vimeripoti kuwa watuhumiwa hao wanaweza kuwa raia wa eneo la kusini mwa Lebanon, lakini hadi sasa hakuna uthibitisho rasmi kuhusu majina yao wala chanzo halisi cha fedha hizo.

Tukio hili limezua maswali mengi kuhusu asili ya fedha hizo na uhusiano wake na mitandao ya usafirishaji haramu wa fedha barani Afrika na Mashariki ya Kati. Mamlaka za Lebanon zinaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na nchi nyingine ili kubaini ukweli wa sakata hili.

Habari hii imeandaliwa na MANGWA