Baraka Juu ya Damu: Nangaa Abarikiwa, AFC Yaendelea Kuua

Ni tukio lililowaacha Wacongo wengi wakitetemeka kwa hasira na masikitiko. Jumatano hii, tarehe 9 Julai 2025, wakati wa ibada maalum ya kumtakasa mfiadini Bwana Chui, Corneille Nangaa — aliyewahi kuwa Rais wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) na sasa ni kiongozi tata wa kisiasa na kijeshi — alipokea baraka za hadhara kutoka kwa maaskofu wakuu watatu wa Kanisa Katoliki.

Askofu Mkuu Fulgence Muteba wa Lubumbashi (na Mwenyekiti wa CENCO), Askofu Willy Ngumbi wa Goma, na Askofu Léonard Kakudji wa Kamina, walimwekea mikono mtu ambaye leo hii anahusishwa moja kwa moja na machafuko yanayoletwa na kundi la waasi la Alliance Fleuve Congo (AFC), linaloshirikiana na waasi wa M23 na linalotuhumiwa kwa mauaji ya halaiki, ubakaji, uporaji na kusababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao mashariki mwa Congo.

Wakati ripoti kutoka Umoja wa Mataifa, MONUSCO, na mashirika ya kiraia zikieleza kwa kina ukatili wa AFC, kitendo hiki cha baraka kwa Nangaa kimeibua swali zito: Je, Kanisa Katoliki limeamua kimya kimya au kwa makusudi kumbariki mmoja wa wanaotajwa kuwa waasisi wa machafuko yanayoitesa DRC?

Corneille Nangaa, ambaye sasa ni mshirika wa kisiasa wa M23 kupitia AFC, amekuwa akikana kuhusika moja kwa moja na machafuko. Lakini matamshi yake ya hadhara yanayohamasisha mapinduzi ya silaha yameenea mitandaoni, yakifichua ajenda yake inayoungwa mkono na mataifa ya jirani kama Rwanda na Uganda — jambo linaloonekana kuwa tishio kwa mamlaka ya kitaifa ya DRC.

Katika hali hiyo, kuonekana kwa viongozi wa juu wa Kanisa wakimbariki hadharani Nangaa limeonekana na wengi kama fedheha ya kitaifa. Hii ni hasa ikizingatiwa kuwa CENCO yenyewe iliwahi kulaani vikali uvamizi wa Rwanda na kutaka amani irejee mashariki mwa nchi.

Kitendo hiki kimeibua maswali kuhusu msimamo wa sasa wa Kanisa Katoliki katika taifa ambalo bado linaota matumaini ya kupata amani ya kudumu. Je, ni mkakati wa kidiplomasia wa kuwa katikati? Ni jaribio la kupoza moto? Au ni upofu wa kisiasa? Kwa raia wa Kongo, hii inaonekana kuwa usaliti wa kimya kimya.

Maana, wakati Nangaa anabarikiwa mjini Goma, huko Rutshuru, miili ya waathiriwa wa AFC inaendelea kuzikwa kimyakimya.

Mwandishi: MANGWA