FDLR Yatoa Barua kwa Rais wa Marekani, Yaeleza Msimamo Wake Kuhusu Amani ya Maziwa Makuu

Tarehe 2 Julai 2025, kikundi cha Forces Démocratiques de Libération du Rwanda (FDLR) kimemwandikia barua Rais wa Marekani, kikieleza msimamo wao wa kuunga mkono makubaliano ya amani yaliyosainiwa mjini Washington tarehe 27 Juni 2025 kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda.

Katika barua hiyo, FDLR imempongeza Rais Donald Trump kwa juhudi zake za kufanikisha makubaliano hayo na kuonyesha nia ya dhati ya kushiriki katika jitihada za kurejesha amani ya kudumu katika Ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika.

FDLR imeeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, imekuwa ikilenga kulinda wakimbizi wa Kinyarwanda walioko mashariki mwa Congo na haijawahi kuwa tishio kwa raia wa Rwanda kama inavyodaiwa na serikali ya Kigali. Kikundi hicho kimedai kuwa shutuma za kuwa kundi la kigaidi au la kijinai ni propaganda ya Rwanda ili kuficha maovu ya kivita yaliyofanywa na serikali ya Kigali katika ukanda huo.

Katika barua hiyo, FDLR imetaja juhudi mbalimbali walizowahi kushiriki katika kutafuta amani, ikiwemo makubaliano ya Rome (2005), mazungumzo ya Goma (2008), na mikutano na serikali ya DRC pamoja na MONUSCO. Wamedai kuwa Rwanda imekuwa ikisusia na kuharibu jitihada hizo zote.

FDLR imekosoa vikali operesheni za kijeshi zilizowahi kufanywa na vikosi vya FARDC, RDF, na MONUSCO dhidi yao, wakidai kuwa mashambulizi hayo yalikuwa sehemu ya njama ya kuwaangamiza wakimbizi wa Kinyarwanda walioko mashariki mwa DRC.

Aidha, kikundi hicho kimeeleza kuwa kulazimishwa kurudi Rwanda kwa wapiganaji wake waliokuwa wamejisalimisha kulifanyika kwa ukatili na hila za kisiasa, ambapo baadhi yao walirubuniwa na kuingizwa katika jeshi la Rwanda na kurudishwa Congo kama wapiganaji wa RDF.

FDLR imesisitiza kuwa suluhisho la mgogoro wa Rwanda na ukanda wa Maziwa Makuu haliwezi kupatikana kwa nguvu za kijeshi bali kupitia mazungumzo ya kina, ya wazi, na ya pamoja kati ya pande zote husika.

Katika hitimisho lake, FDLR imetangaza kuwa ipo tayari kushiriki katika mchakato wa amani, kuunga mkono jitihada zote za kuleta utulivu, na inalenga kuhakikisha usalama wa wakimbizi wa Kinyarwanda walioko mashariki mwa Congo hadi warudi nyumbani kwa heshima na usalama.

Barua hiyo pia imetumwa nakala kwa viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, na mashirika ya kikanda kama SADC na EAC.