Kagame: Rwanda Imejitolea Kutekeleza Mkataba wa Amani wa Washington

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amesema nchi yake iko tayari kutekeleza kikamilifu makubaliano ya amani yaliyotiwa saini hivi karibuni mjini Washington kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Akizungumza na vyombo vya habari, Kagame alieleza kuwa Rwanda itaendelea kuheshimu kile walichokubaliana katika mkataba huo wa kihistoria.

“Naweza kusema kwa upande wa Rwanda tutafanya yale tuliyokubaliana kadri tuwezavyo, lakini mengine inategemea na wengine watafanya nini na sisi tumekubali kufanya,” alisema Kagame.

Kauli hii inakuja baada ya miezi ya mvutano na mapigano katika maeneo ya mashariki mwa Congo, ambapo kundi la waasi la M23 linaendelea kudhibiti sehemu kubwa ya ardhi, huku likihusishwa na msaada wa Rwanda – madai ambayo Kigali imekuwa ikikanusha vikali.

Mkataba wa Washington unaelekeza hatua muhimu kama vile kusitisha mapigano, kuondoa vikosi vya Rwanda kwenye ardhi ya Congo, na kushirikiana katika kurudisha wakimbizi pamoja na kupokonya silaha makundi ya waasi yanayohusika na machafuko.

Serikali ya Congo imeeleza matumaini kuwa Rwanda itaheshimu vipengele vya mkataba huo na kwamba pande zote zitachangia kuleta amani ya kudumu kwa manufaa ya wananchi wa eneo la Maziwa Makuu.

Mazungumzo ya utekelezaji wa mkataba huo bado yanaendelea huku jumuiya ya kimataifa ikifuatilia kwa karibu hatua zitakazochukuliwa na pande zote.