Nangaa Aondolewa Katika Uongozi wa AFC/M23 Kwa Kutuhumiwa Kuwa na Malengo Binafsi

Kigali – Corneille Nangaa, aliyewahi kuwa Rais wa Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC), ameondolewa katika nafasi yake ya uongozi ndani ya muungano wa waasi wa AFC/M23, baada ya Rwanda kumtuhumu kuwa na malengo binafsi ya kulazimisha kuchukua madaraka kwa njia ya kijeshi.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya siri kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumatano, tarehe 2 Julai 2025, Nangaa anatuhumiwa kuwa na hamu kubwa ya kuvamia Kinshasa na kupindua serikali kuu – jambo ambalo Rwanda, licha ya kuunga mkono mabadiliko ya uongozi, halikuwa tayari kulitumia nguvu za kijeshi kufanikisha.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa awali, Nangaa alichukuliwa kama sura ya kisiasa ya harakati za AFC/M23, akitumiwa na Kigali “kutoa mwonekano wa muungano wa kitaifa” kwa kundi hilo lililotuhumiwa kuongozwa na Rwanda. Hata hivyo, msimamo wake mkali wa kutaka kuingia Kinshasa kwa mabavu ulipingwa vikali na washirika wake wa Rwanda, ambao walichagua kubaki na mikakati ya kijeshi ndani ya mashariki ya Congo pekee.

Uongozi wa AFC/M23 Waangaziwa

Kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, uongozi wa kijeshi wa waasi wa AFC/M23 unaendelea kuwa chini ya Jenerali Sultani Makenga, huku upande wa kisiasa ukiwa mikononi mwa Bertrand Bisimwa na, kwa jina tu, Corneille Nangaa. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa maamuzi muhimu yanaendelea kufanywa Kigali, chini ya ushauri wa maofisa waandamizi wa Rwanda kama Fred Ngenzi Kagorora na Jenerali Patrick Karuretwa, wanaodaiwa kudhibiti mawasiliano ya moja kwa moja na viongozi wa waasi.

Tangu kurejea kwa M23 mnamo Novemba 2021, kundi hilo limepanuka haraka na kwa muda mfupi lilidhibiti miji mikuu ya mikoa miwili ya mashariki: Goma na Bukavu. Hatua hii imeongeza shinikizo kwa serikali ya Kinshasa ambayo jeshi lake limekuwa likihangaika kuzuia kasi ya waasi.

Wananchi Wapinga Mbinu za AFC/M23

Licha ya mafanikio ya kijeshi ya AFC/M23, wananchi wengi wa Congo wanapinga harakati hizi, wakiziona kuwa ni njama za nje za kuivuruga nchi na kuipora mali asili zake. Mbinu ya kutumia nguvu kumtoa serikali iliyoko madarakani imeendelea kukataliwa vikali na Wacongo waliowengi.

Hali hii inazidi kudhihirisha kuwa mgogoro wa mashariki mwa Congo hauhusiani tu na siasa za ndani, bali ni vita vya kanda vinavyochochewa na maslahi ya mataifa jirani.

Mwisho wa Habari

Mwandishi: MANGWA