
Adolphe Muzito Ampongeza Rais Tshisekedi kwa Hatua za Kidiplomasia na Kazi ya Kujenga Taifa
🔴 Kinshasa, Jumatano 2 Julai 2025 — Katika tukio la kihistoria lililofanyika leo katika Cité de l’Union africaine, Kinshasa, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, amekutana kwa mara ya kwanza na aliyekuwa Waziri Mkuu na Kiongozi wa chama cha upinzani Nouvel Élan, Adolphe Muzito.
Baada ya mazungumzo yao, Adolphe Muzito alieleza kuwa walijadili kwa kina kuhusu hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi. Muzito alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Tshisekedi kwa mafanikio aliyoyapata katika medani ya kimataifa.
“Tulimshukuru kwa matokeo chanya aliyoyapata. Zamani alikosolewa kwa kusafiri sana nje ya nchi, lakini leo tumeona matunda yake: kufanikisha kuitangaza kimataifa kuwa Rwanda ndiye mvamizi wa DRC kupitia waasi wake, pamoja na kusimamia kusainiwa kwa mkataba chini ya usimamizi wa Marekani unaowataka Rwanda na waasi kujiondoa katika ardhi ya Congo,” alisema Muzito.
Aidha, Muzito alimsifu Rais Tshisekedi kwa mafanikio ya kiuchumi, hasa kwa kufanikisha makubaliano yanayotarajiwa kati ya DRC na Marekani, ambayo yataleta mabadiliko katika usimamizi wa rasilimali za nchi.
“Kile kilichokuwa kinaporwa na Rwanda kama wakala wa mataifa mengine sasa Congo itakimiliki na kushirikiana na mataifa yote duniani, hususan Marekani,” aliongeza.
Muzito alisisitiza kuwa ni kawaida kwa mkataba huo kuibua mjadala miongoni mwa wananchi na kwamba serikali inapaswa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu makubaliano hayo.
Kuhusu ushiriki wake katika serikali ya umoja wa kitaifa, Muzito alisema: “Nimesema niko tayari kushiriki katika kuunda serikali hiyo. Ni muhimu mawazo yangu yazingatiwe kadri inavyowezekana.”
Mwisho wa mazungumzo yao, Muzito alimshauri Rais Tshisekedi kuandaa mazungumzo ya kitaifa au kuanza haraka mchakato wa mageuzi makubwa yatakayoipeleka nchi mbele.




Mwandishi: Mangwa
