
Ndege Isiyojulikana Yakiuka Anga la Congo, Jeshi Latekeleza Hatua za Dharura
Jumatatu, tarehe 30 Juni 2025, katika siku ya kumbukumbu ya Uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jeshi la Congo (FARDC) limethibitisha kugundua ndege isiyojulikana iliyokiuka anga la taifa bila kibali rasmi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi la Congo, Jenerali Sylvain Ekenge Bomusa, ndege hiyo ilionekana kupitia rada za kijeshi ikisafiri kuelekea katika eneo la vita mashariki mwa nchi bila ruhusa ya kuingia katika anga la Congo.
“Jeshi la Congo lipo macho kila wakati kulinda anga lake. Ndege hiyo haikuwa na namba ya usajili na haikutambulika na vyombo vya anga vya kimataifa. Ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za anga duniani,” alisema Jenerali Ekenge.
Jeshi limechukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wa taifa na kudhibiti tukio hilo. Uchunguzi wa kina umeanzishwa ili kubaini chanzo na mmiliki wa ndege hiyo pamoja na kusudi la safari yake.
“Hatutaruhusu mtu yeyote kuvunja mipaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tunalinda ardhi, anga na raia wetu kwa ujasiri na nguvu zote,” aliongeza msemaji huyo.
FARDC imesisitiza kuwa iko tayari kujibu kwa ukali vitendo vyovyote vinavyotishia mamlaka ya taifa hilo. Ripoti zaidi za matokeo ya uchunguzi zinatarajiwa kutolewa hivi karibuni.
Mwandishi: MANGWA
