Burundi: Viongozi wa Upinzani Walio Uhamishoni Watangaza Kuandaa Mapambano ya Kijeshi Baada ya Kudai Wizi wa Kura

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mwishoni mwa wiki hii mjini Brussels, Ubelgiji, baadhi ya wanasiasa wa Burundi walio uhamishoni wametangaza kuwa wako katika maandalizi ya kuchukua silaha kupinga kile walichokiita wizi wa kura katika uchaguzi uliopita, wakisema kuwa uchaguzi huo umefungua milango ya kuharibu nchi.

Frederique Bamvuginyumvira, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Burundi, na ambaye sasa ni mmoja wa wanasiasa wanaoishi uhamishoni, amesema kuwa hawana chaguo jingine zaidi ya kuingia vitani ili kuikomboa Burundi.

“Tumeona uchaguzi ukiibiwa waziwazi. Watu wamelazimishwa kupiga kura, wengine wameporwa kadi zao za kupigia kura, na wengine wamepiga kura kwa nguvu. Hali hii haiwezi kuvumilika. Chama kilichopo madarakani kimeleta mateso kwa wananchi, tumeamua kuchukua silaha na kupigania uhuru wa nchi yetu. Hawa wanataka kutuua, lakini sisi tumeamua kupigana kwa pinde na mishale,” alisema Bamvuginyumvira.

Ingawa hakutaja jina la kikundi chao au nani hasa atakuwa sehemu ya harakati hizi, alisisitiza kuwa kuchukua silaha sasa ni njia isiyoepukika. Aliongeza kuwa watu wanaojiunga na harakati hii ya ukombozi wanapatikana ndani na nje ya Burundi.

Wanasiasa hao wanatoka katika makundi matatu ya kisiasa ambayo ni:

  • Cfor Arusha (Muungano wa Vikosi vya Upinzani vya Burundi kwa Marejesho ya Mkataba wa Arusha)
  • CN (Coalition for the Renaissance of the Nation), inayowakilishwa na Chauvinau Mugwengezo
  • Patriotic Action Movement, inayowakilishwa na msemaji wake Liberat Ntibashirakandi.

Viongozi hao wamesema wamejaribu zaidi ya mara nane kuingia kwenye mazungumzo ya kisiasa na kutumia njia za kidiplomasia bila mafanikio yoyote. Hivyo, sasa wanaamini kuwa njia pekee ya kusikika ni kupitia mapambano.

“Hatuna imani tena na programu za mazungumzo. Tumejaribu mara nyingi lakini serikali imetufungia milango yote. Njia pekee iliyobaki ni vita vya ukombozi,” alisema Bamvuginyumvira.

Hadi sasa, serikali ya Burundi haijatoa tamko rasmi kuhusu tishio hili la upinzani walio uhamishoni.

Habari hii imeandaliwa na MANGWA