Rais Félix Tshisekedi: “Rasilimali za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Haziwezi Kamwe Kuuzwa kwa Bei ya Hasara”
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC), Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, ametoa kauli kali akisisitiza kuwa rasilimali za nchi hiyo hazitawahi kuuzwa kwa bei ya hasara wala kukabidhiwa kwa maslahi ya kutiliwa shaka.
Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Rais Tshisekedi alisema wazi:
“Rasilimali za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haziwezi kamwe kuuzwa wala kukabidhiwa kwa maslahi yenye mizania isiyoeleweka au kwa mikataba yenye kivuli.”
Kauli hii inakuja wakati ambapo mazungumzo na makubaliano kadhaa ya amani na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Congo na Rwanda yamezua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi na viongozi wa vyama vya upinzani.
Rais Tshisekedi amesisitiza kuwa mkataba wa hivi karibuni uliotiwa saini mjini Washington hautahatarisha wala kuathiri uhuru wa kiuchumi wa taifa. Ametoa wito kwa wananchi kupuuza uvumi na propaganda zinazoenezwa kuwa serikali yake imekubali kuuza au kugawa rasilimali za nchi kwa mataifa ya nje.
“Ninawahakikishia wananchi wa Congo: sisi kama serikali tutaendelea kulinda ardhi yetu, uhuru wetu na rasilimali zetu kwa maslahi ya watu wetu,” alisema Rais Tshisekedi.
Viongozi wa serikali wameeleza kuwa makubaliano ya Washington yamelenga kuimarisha amani, kurejesha usalama katika maeneo yaliyoathirika na vita, pamoja na kuanzisha ushirikiano wa haki wa kibiashara baina ya mataifa ya ukanda huu.
Wananchi wengi wamepokea kauli ya Rais Tshisekedi kama ujumbe wa kuimarisha umoja wa kitaifa na kulinda utajiri wa nchi, hasa baada ya miongo kadhaa ya migogoro ya kijeshi na uporaji wa rasilimali.
Habari hii imeandaliwa na MANGWA
