
MAKUBALIANO YA AMANI YA WASHINGTON YAZUA MJADALA MKALI KATI YA SERIKALI YA CONGO NA RWANDA
Makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda huko Washington yameibua maoni tofauti nchini Congo, huku baadhi ya viongozi wakilalamikia mkataba huo kuwa ni wa kibiashara zaidi kuliko wa kuleta amani ya kweli.
Rais wa zamani wa Congo, Joseph Kabila, ameonyesha kutoridhishwa na mkataba huo akisema, “Si chochote zaidi ya makubaliano ya kibiashara.” Kabila anaamini kuwa mkataba huo haujazingatia maslahi ya usalama wa nchi, bali umelenga zaidi kuruhusu biashara ya madini kati ya Congo na mataifa ya nje, hususan Marekani.
Makubaliano hayo, yaliyosainiwa Ijumaa iliyopita, yanataka “kutengwa, kupokonywa silaha na kuunganishwa kwa masharti” kwa vikundi vyote vyenye silaha vinavyohusika kwenye mapigano mashariki mwa Congo, lakini maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wake bado hayajatolewa wazi.
Wakati huo huo, baadhi ya viongozi wa kimataifa na wanadiplomasia wamepongeza hatua hiyo kama mwanzo wa mchakato wa kudumu wa kurejesha amani katika eneo hilo linalokumbwa na vita vya muda mrefu.
Rwanda, kupitia maafisa wake wa juu, imeendelea kupinga madai kuwa inatoa msaada kwa waasi wa M23 wanaodaiwa kusababisha machafuko makubwa mashariki mwa Congo. Hata hivyo, ushahidi wa Umoja wa Mataifa umeonyesha ushiriki wa Rwanda katika vita hivyo, madai ambayo Kigali imeyakanusha vikali.
Mzozo huu ulizidi kushika kasi mapema mwaka huu baada ya waasi wa M23 kuchukua maeneo makubwa ya mashariki mwa Congo, yakiwemo mji wa Goma, Bukavu, na viwanja viwili vya ndege muhimu katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, maelfu ya watu wameuawa na mamia kwa maelfu kulazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi hayo. Hata hivyo, kundi la M23 limekanusha takwimu hizo na kudai kuwa idadi ya waliopoteza maisha ni chini ya watu 1,000.
Baada ya kupoteza udhibiti wa maeneo hayo, Serikali ya Congo iligeukia Marekani kwa msaada wa kiusalama na taarifa zinaeleza kuwa nchi hiyo ilikubali kutoa upatikanaji wa madini muhimu kwa ajili ya usalama wa taifa lake. Mashariki mwa Congo ina utajiri mkubwa wa madini adimu kama coltan ambayo ni kiungo muhimu katika utengenezaji wa vifaa vya elektroniki duniani.
Makubaliano haya ya Washington yanaendelea kufuatiliwa kwa karibu na raia wa Congo, wakiwemo wanaharakati wa kiraia na viongozi wa kisiasa, wakitaka uwazi kuhusu vipengele vya mkataba huo na kuhakikisha kuwa heshima ya nchi na usalama wa wananchi vinawekwa mbele kuliko maslahi ya kiuchumi ya mataifa ya nje.
Habari hii imeandaliwa na MANGWA
