
Daktari Denis Mukwege Aonyesha Wasiwasi Kuhusu Makubaliano ya Amani Kati ya Rwanda na Kongo
Daktari Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na mtetezi mkubwa wa haki za waathiriwa wa ukatili wa kingono nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu makubaliano ya hivi karibuni yaliyosainiwa kati ya Rwanda na Kongo.
Katika taarifa yake, Dkt. Mukwege amesema kuwa mkataba huu unatoa faida kubwa kwa Rwanda na Marekani, huku ukiyaacha bila majibu madai ya msingi ya haki kutoka kwa waathiriwa wa uvamizi, uporaji wa rasilimali, na ukatili uliodumu kwa miongo kadhaa mashariki mwa Kongo.
“Hatuwezi kuzungumzia amani ya kweli bila haki kwa waathiriwa. Makubaliano yoyote ambayo yanapuuza maumivu ya watu wetu na kuwapa nafasi wanaodhaniwa kuwajibika, hayawezi kuwa suluhisho la kudumu,” alisema Mukwege.
Dkt. Mukwege aliongeza kuwa upatanishi wa aina hii unaweza kuonekana kama kufumbia macho uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu ambao umetendeka mashariki mwa Congo.
Wakati viongozi wa kimataifa wanapongeza makubaliano haya kama fursa ya kuleta utulivu wa kikanda na kufungua milango ya uwekezaji wa madini muhimu, Mukwege anasisitiza kuwa amani bila haki ni msingi wa mgogoro wa baadaye.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapewa sauti na kwamba kuna mchakato wa wazi wa kuwawajibisha wote waliotenda uhalifu,” alisema.
Daktari Mukwege, ambaye amekuwa mstari wa mbele kusaidia wanawake waliobakwa katika migogoro ya Kongo, amekuwa sauti ya dunia akitaka kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kuendesha kesi za uhalifu wa kivita nchini Kongo.
Wito wa Haki na Uwajibikaji
Mukwege anatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa makubaliano haya yanajumuisha haki kwa waathiriwa, hatua madhubuti za kusitisha uporaji wa rasilimali, na uwazi katika utekelezaji wa vipengele vyote vya mkataba.
Katika kipindi ambapo matumaini ya amani yanaonekana kuongezeka, Mukwege anakumbusha kuwa bila mizizi ya haki, msingi wa amani unaweza kuwa dhaifu sana.
✍️ Mwandishi: MANGWA
#DRC #Rwanda #Amani #DenisMukwege #Haki #M23
