Tanzania Bara: Yanga SC Yatwaa Ubingwa wa 31 Katika Ligi Iliyojaa Maswali na Sintofahamu

Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2024/2025 umehitimishwa kwa namna ya kipekee lakini yenye utata mkubwa. Klabu ya Yanga SC imeandika historia nyingine baada ya kutwaa ubingwa wake wa nne mfululizo na wa jumla wa 31, kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wa mwisho uliofanyika Juni 25, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Licha ya mafanikio haya, msimu huu umeacha doa kubwa kwenye soka la Tanzania, huku taswira ya ligi ikiwa imetikisika kutokana na mfululizo wa matukio yaliyoibua maswali kuhusu utawala, uwazi na uadilifu wa Bodi ya Ligi, TFF, na wadau wa soka nchini.

Sakata la Dabi ya Kariakoo: Chanzo cha Sintofahamu

Maandalizi ya mechi ya dabi ya Kariakoo (namba 184) iliyopangwa kufanyika Machi 8, 2025 yaligeuka kuwa kitendawili kikubwa. Simba SC walidai kunyimwa haki yao ya kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, na kulingana na taarifa kutoka Simba, walizuiwa kuingia uwanjani kwa makusudi, jambo lililoathiri maandalizi yao.

Taarifa zilianza kuenea kwamba sababu ya kuzuia mazoezi ilikuwa ni imani za kishirikina, huku pande zote mbili zikitupiana lawama kuhusu kuingiza ushirikina kwenye mchezo huo.

Simba SC walikosa imani na mazingira ya mchezo na wakaamua kutohudhuria mechi hiyo, jambo lililosababisha Bodi ya Ligi (TPLB) kuahirisha mechi hiyo kwa muda usiojulikana. Mchezo huo ulipangwa tena Juni 15, 2025, lakini ulifanyika chini ya kivuli cha sintofahamu kubwa.

Madai ya Muda Mrefu: Siri ya “Simu ya Serikali”

Katika kikao cha suluhu kilichoitishwa kujadili hatma ya mechi hiyo, Msemaji wa Yanga SC, Ally Kamwe, alitoa madai mazito kuwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo, alikiri kuwa kulikuwa na “simu ya kiongozi mkubwa wa serikali” aliyetoa maelekezo ya kufunga geti la uwanja ili kuzuia mazoezi ya Simba SC.

Hata hivyo, jina la kiongozi huyo halikutajwa, na tangu hapo, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusiana na tukio hilo, jambo ambalo limeongeza sintofahamu.

Nini Hatma ya Ripoti ya Uchunguzi?

Licha ya ahadi ya Bodi ya Ligi kuchunguza tukio hilo, hakuna ripoti iliyotolewa hadharani hadi leo. Taarifa kuhusu uchunguzi huo zimefichwa, huku viongozi wakuu wa TFF na TPLB wakikaa kimya.

Hata baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto, na kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu Almasi Kasongo, bado majibu yanakosekana.

Maswali Muhimu Bado Yamebaki:

  • Nini kilitokea Machi 8, 2025?
  • Kwa nini Simba SC walizuiwa kuingia uwanjani?
  • Nani alihusika kutoa agizo hilo?
  • Kwa nini ripoti ya uchunguzi haijawahi kutolewa hadharani?

Mwisho wa Msimu Bila Majibu

Ubingwa wa Yanga SC msimu huu umepatikana katika mazingira yaliyoacha doa kubwa kwenye heshima ya ligi. Wadau wa soka, wachambuzi, na mashabiki wanaendelea kuhoji uadilifu wa usimamizi wa ligi hiyo.

“Hii ni doa la kiutawala ambalo linapaswa kusafishwa kwa uwazi,” alisema Rahman John, mfuatiliaji wa soka la Tanzania na shabiki wa Yanga.

Kwa sasa, jicho la mashabiki limeelekezwa kwa Bodi ya Ligi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutoa ripoti ya uchunguzi wa sakata hili ili kusafisha taswira ya ligi na kurejesha imani ya wadau wa soka nchini.

Muandishi: MANGWA

#TanzaniaBara #YangaSC #SimbaSC #DabiYaKariakoo #TPLB #TFF #HabariZaSoka #MCMR