🔴 BUKAVU: Hali ya Usalama Bagira Yazidi Kuzorota, Maelfu Wakimbia Mapigano Kati ya Wazalendo na AFC/M23

Bagira, Sud-Kivu – Hali ya usalama katika mji wa Bukavu, hasa katika eneo la Bagira, imekuwa ya kutisha kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya wapiganaji wa Wazalendo na wanajeshi wa kundi la AFC/M23 katika maeneo ya Kabare.

Kwa siku kadhaa sasa, vijiji kadhaa vimebaki vitupu kutokana na wimbi kubwa la wakazi waliolazimika kukimbia makazi yao katika maeneo kama Cirunga, Bushwira, Mulege, na Muganda. Wengi wa wakimbizi hawa wameelekea katika mtaa wa Bagira, wakiomba hifadhi kwa familia za wakazi wa mji huo wakitafuta amani na usalama wa muda.

Shuhuda wa tukio, Bw. Guilain Kanyena, mwanaharakati wa jamii kutoka tawi la Lumumba, amesema hali hii ni mbaya na huenda ikawa ya kutisha zaidi siku zijazo endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa mara moja.

“Watu wanakimbia vita wakiwa hawana chochote. Wameacha kila kitu nyuma yao, na sasa wanahangaika kutafuta chakula na makazi. Hali hii ya uhamiaji wa ghafla pia inaleta changamoto mpya ya usalama wa chakula pamoja na usalama wa kawaida ndani ya Bagira,” alisema Bw. Kanyena.

Ametoa wito kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu kuingilia kati haraka na kuleta msaada wa dharura kwa wakimbizi hawa wa vita, akiongeza kuwa jamii ya Bagira inaweza kufikia kikomo cha uwezo wa kuwahudumia wakimbizi hawa iwapo hakutakuwa na msaada wa nje.

Hali ya sintofahamu na hofu imetanda miongoni mwa wakazi wa Bagira huku wengi wakihofia kuibuka kwa migogoro mipya ya kiusalama ndani ya mji kutokana na ongezeko la wakimbizi wasiojulikana kikamilifu.

Muandishi: MANGWA

#SudKivu #Bagira #Wazalendo #M23 #Bukavu #HabariZaLeo #MCMR