
🔴 RDC : Wananchi Walalamikia Ugumu wa Kupata Pasipoti Mpya ya Biometriki
Kinshasa, 26 Juni 2025 – Zaidi ya wiki mbili baada ya uzinduzi rasmi wa pasipoti mpya ya biometriki kwa bei ya dola 75 za Kimarekani, raia wengi wa Congo bado wanakumbana na changamoto kubwa kupata hati hiyo muhimu ya kusafiria.
Ingawa wananchi wengi wameshalipa ada husika na kukamilisha hatua zote za taratibu za maombi, mamia ya waombaji wanaendelea kurudi nyumbani mikono mitupu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje kila siku, bila kupata majibu.
Kupunguzwa kwa bei ya pasipoti kumewafanya watu wengi kufurika katika vituo vya usajili, lakini mchakato wa utoaji wa pasipoti unaonekana kusuasua na kushindwa kuendana na mahitaji ya wananchi.
“Mwanangu mwenye umri wa miaka 18 alishamaliza hatua ya kuchukuliwa alama za vidole na picha, lakini tangu hapo hatujasikia chochote. Tumeambiwa kampuni ya zamani imezuia taarifa,” alisema mama mmoja aliyehojiwa na Radio Okapi.
Hali hii imezua taharuki miongoni mwa waombaji ambao walitarajia kupata huduma kwa haraka kufuatia uzinduzi wa mfumo mpya wa pasipoti. Watu wengi sasa wanatoa wito kwa serikali kuhakikisha ufanisi wa mfumo huu mpya ili kutimiza matarajio ya wananchi.
Muandishi: MANGWA
#RDC #PasipotiBiometriki #HudumaKwaWananchi #ChangamotoZaPasipoti
