
🔴 KENYA: Idadi Kubwa ya Polisi Yashuhudiwa Nairobi Siku ya Maandamano ya Kumbukumbu ya Mwaka Mmoja wa Kupinga Mswada wa Fedha wa 2024
Idadi kubwa ya polisi imeshuhudiwa jijini Nairobi na maeneo mengine nchini Kenya siku ya Jumatano, Juni 26, 2025, wakati Wakenya wakijiandaa kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufanyika kwa maandamano makubwa ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.
Maandamano haya mapya, yaliyoitishwa na wanaharakati na mashirika ya kiraia, yanalenga kulaani ukatili wa polisi na kudai uwajibikaji wa vikosi vya usalama.
Kulingana na taarifa ya Citizen Online, barabara kuu za kuingia katikati ya jiji la Nairobi zilifungwa mapema asubuhi, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri waliolazimika kushuka katika vituo vya mbali na kutembea kwa miguu kufika katikati mwa mji.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, pamoja na maafisa waandamizi wa usalama, walifika Harambee House saa 5:30 asubuhi kufuatilia hali ya usalama na kujadili hatua za kuhakikisha utulivu katika maeneo ya maandamano.
Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, aliwataka waandamanaji kuheshimu sheria na kuepuka maeneo yaliyopigwa marufuku.
“Maafisa wa usalama watachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ili kulinda maisha na mali za raia,” alisema IG Kanja, akifuatana na maafisa wakuu wa usalama wakiwemo Mkurugenzi wa DCI Amin Mohamed, Kamanda wa GSU Ranson Lolmodoni, na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nairobi George Seda.
Kanja hakujibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kutoa tamko lake, lakini alisisitiza kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi iko tayari kuwezesha maandamano halali kwa mujibu wa sheria, huku akionya vikali dhidi ya vitendo vya uchochezi au uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Nairobi George Seda alithibitisha kuwa jeshi la polisi limepokea taarifa rasmi kuhusu maandamano hayo na limejiandaa kikamilifu kuhakikisha amani na usalama vinadumishwa jijini Nairobi na maeneo mengine ya nchi.
Taarifa zaidi zinasubiriwa kadri hali inavyoendelea kufuatiliwa.
Muandishi: MANGWA
#HabariKenya #MaandamanoNairobi #UsalamaKenya
