Uvira, 23 Juni 2025 – Katika taarifa kali iliyotolewa mjini Uvira, kundi la Wazalendo limepinga vikali matamshi ya Jenerali wa Uganda, Muhoozi Kainerugaba, aliyewaita kuwa “nguvu hasi” kufuatia mkutano wake na Rais Félix Tshisekedi huko Kinshasa.

Wazalendo, wanaojitambulisha kama sehemu ya Jeshi la Akiba la Ulinzi wa Taifa (RAD), wamesisitiza kuwa wao ni raia wazalendo wanaojitolea kulinda mamlaka na uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

“Wazalendo wanakataa kunyenyekea kwa aibu na fedheha ambayo serikali ya Congo imekuwa ikivumilia kwa muda mrefu. Tuko tayari kwa sadaka ya mwisho ili kutimiza wajibu wetu wa kikatiba. Tunatoa wito kwa raia wengine kutimiza wajibu wao kama inavyoelekezwa kwenye vifungu vya 63 na 64 vya Katiba yetu,” taarifa hiyo imesema.

Wazalendo pia wamelaani vikali jaribio lolote la kuingiliwa na mataifa ya kigeni na jitihada za kuwapotosha kama watu wasio halali. Wamekumbusha kuwa vuguvugu lao lilizaliwa kutokana na haja ya kujilinda dhidi ya uvamizi wa mataifa ya kigeni tangu mwaka 1996.

“Kauli ya mtoto wa Rais Museveni ya kutaka kuwadhibiti raia wa Congo kwenye ardhi yao wenyewe ni tishio la moja kwa moja kwa uhuru wa Congo. Wazalendo wamesimama kwa haki ya kujilinda mbele ya majeshi ya kigeni, yakiwemo yale ya Uganda tangu 1996,” imeeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Dr. Amb. Doudou Mirefu.

Kwa habari zaidi, mecamediaafrica.com

Muandishi: MANGWA

#MANGWA