Kinshasa, Jumamosi 21 Juni 2025 — Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC), Félix Tshisekedi, leo amekutana na Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Majeshi na Kamanda wa Jeshi la Uganda (UPDF), katika mkutano uliofanyika kwenye Cité de l’Union Africaine jijini Kinshasa.

Ziara ya Jenerali Muhoozi nchini DRC, iliyoanza Ijumaa iliyopita, ni sehemu ya kikao cha tathmini ya operesheni ya kijeshi ya pamoja kati ya majeshi ya FARDC (Jeshi la Congo) na UPDF, akishirikiana na mwenzake wa Congo, Jenerali Jules Banza Mwilambwe.

Katika mazingira ya heshima ya kijeshi na kidiplomasia, Jenerali Muhoozi alitumia fursa hiyo kutoa salamu za heshima kwa Rais Félix Tshisekedi, ambaye ndiye Kamanda Mkuu wa Majeshi ya FARDC. Mazungumzo yao yalihusu maendeleo ya operesheni ya pamoja, hali ya usalama mashariki mwa DRC, na kuimarisha uhusiano wa kijeshi kati ya nchi hizo jirani.

Mkutano huu unaonesha mwendelezo wa juhudi za pamoja kati ya DRC na Uganda katika kupambana na makundi ya waasi, hasa ADF, yanayosababisha ukosefu wa usalama kwenye mpaka wa nchi hizo mbili.

Taarifa kamili kuhusu maazimio ya tathmini hiyo ya kijeshi inatarajiwa kutolewa katika siku chache zijazo.

✍🏽 Mwandishi: MANGWA

#FARDC #UPDF #MuhooziKainerugaba #FelixTshisekedi #Kinshasa #RDCUganda #MecaMedia #MANGWA