
Uvira, 18 Juni 2025 — Hali ya usalama katika komine ya Kalundu, wilaya ndogo ya Songo, imeingia tena kwenye vichwa vya habari baada ya jambazi mmoja kuuawa na kikundi cha Wazalendo, leo jioni majira ya saa 1 (19h), katika avenue Mapendano.
Tukio hilo limetokea baada ya wahalifu watatu kufanya uvamizi katika avenue Démocratie, ambapo walimvamia raia mmoja na kumpora simu kwa nguvu. Baada ya tukio hilo, wahalifu hao walikimbia kwa kasi, lakini mmoja wao alinaswa na kuzingirwa na Wazalendo, na hatimaye akauliwa katika harakati za kutaka kutoroka. Wahalifu wawili waliobaki waliweza kutoroka bila kutambuliwa kuelekea mahali pasipojulikana.
🔴 Wito kwa Serikali
Tukio hili limeibua hofu na mjadala mpana miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku wito ukitolewa kwa mamlaka husika, hasa uongozi wa usalama, kuimarisha doria, kamera za ulinzi, na ufuatiliaji wa maeneo yenye hatari kubwa ya uhalifu.
🎙️ “Tunaishi kwa hofu kila siku, na vijana wanapotea kwa matendo ya kihalifu. Tunahitaji hatua za haraka na za kweli kutoka kwa serikali,” alisema mkazi mmoja wa Songo aliyezungumza na MCMR-RDC.
🔔 Tukio hili linaonesha jinsi raia wanavyochukua sheria mkononi, kutokana na kuchoshwa na matukio ya uhalifu usioisha, lakini pia linatoa ishara ya haja ya marekebisho ya haraka katika mfumo wa usalama wa maeneo ya mijini.
✍️ Mwandishi: MANGWA
📌 #Uvira #Kalundu #Wazalendo #Usalama #HabariZaUvira #MCMRRDC #MecaMedia
