
📍 Kinshasa, 18 Juni 2025 — Katika hatua ya kushangaza iliyogonga vichwa vya habari, Waziri wa zamani wa Sheria, Constant Mutamba, ametangaza kujiuzulu kutoka katika serikali ya Waziri Mkuu Judith Suminwa, serikali aliyohudumu kwa mwaka mmoja.
Katika barua rasmi aliyomwandikia Rais Félix Tshisekedi, Mutamba ameeleza kuwa uamuzi wake umetokana na kile anachokiita “njama ya kisiasa iliyopangwa Kigali na kutekelezwa na baadhi ya Wacongo wenyewe”.
🗣️ “Kama askari wako mtiifu, niliyejitolea kupambana na viongozi wa juu wa AFC/M23, nimeshangazwa sana na kitendo hiki cha usaliti. Njama hii ya kisiasa ilitungwa Kigali na inalenga kuvunja juhudi za mageuzi na uzalendo niliokuwa nao,” ameandika Mutamba.
📉 Ajitetea kuhusu tuhuma za ufisadi
Mutamba amekanusha vikali tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma zinazomkabili kuhusiana na mamilioni ya dola yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa gereza mjini Kisangani.
💬 “Sijawahi kuchukua hata dola moja ya serikali,” amesema kwa msisitizo katika barua hiyo ya kujiuzulu.
📌 Muktadha mpana
Kujiuzulu kwake kunakuja siku chache baada ya Bunge la Taifa kupitisha azimio la kumfungulia mashtaka, kufuatia ripoti ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Rufaa, aliyemtuhumu kwa kuhusika na matumizi mabaya ya zaidi ya Dola milioni 19 za Marekani.
Hatua ya Mutamba inaweza kuwa mwanzo wa mvutano mpya wa kisiasa nchini, hasa ikizingatiwa kauli yake inayohusisha mataifa jirani katika hali ya kisiasa ya ndani ya DRC.
✍️ Mwandishi: MANGWA
📌 #ConstantMutamba #RDC #Ufisadi #Kigali #SiasaZaCongo #MecaMedia

