
Goma, Juni 14, 2025 – Mazungumzo muhimu kati ya uongozi wa kundi la waasi wa AFC/M23 na ujumbe wa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bi Bintou Keita, yamekamilika hii leo katika hoteli ya Serena, mjini Goma.
Vikao hivyo vilianza saa 4:15 asubuhi hadi 7:49 mchana, na kuendelea tena saa 9:36 alasiri hadi 11:58 jioni, yakijadili hali ya usalama na hatima ya mchakato wa amani katika maeneo yanayokumbwa na machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Baada ya kumalizika kwa kikao, Bi Bintou Keita alizungumza na vyombo vya habari, akielezea umuhimu wa mazungumzo hayo katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa mgogoro wa miongo mingi unaohusisha kundi la M23, serikali ya Kongo, na wadau wa kikanda na kimataifa.
“Lengo kuu ni kupunguza mateso ya raia na kusisitiza njia za kisiasa na majadiliano katika kutafuta amani ya kweli,” alisema Bintou Keita mbele ya waandishi wa habari waliokusanyika.
Hata hivyo, hakuna taarifa ya pamoja iliyotolewa na pande mbili kuhusu makubaliano yoyote yaliyofikiwa, jambo linaloashiria kuwa bado kuna hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa katika kuelekea utulivu wa kudumu.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO) unaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama Kivu Kaskazini, huku mashirika ya haki za binadamu yakitoa wito wa kulindwa kwa raia na kusitishwa kwa uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na vikundi vyenye silaha.
✍🏾 Mwandishi: MANGWA
#Goma #M23 #BintouKeita #AmaniMashariki #DRC #MONUSCO #MANGWA
