
Ahmedabad, India – Juni 2025 Ajali ya ndege ya Air India iliyokuwa ikielekea London imeacha huzuni kubwa duniani kote, lakini ni simulizi ya familia moja – ya Pratik Joshi – iliyogusa mamilioni ya watu kwa namna ya kipekee.
Pratik Joshi, raia wa India aliyekuwa akifanya kazi jijini London kwa muda wa miaka sita, alikuwa amejiandaa kwa muda mrefu kuwaleta mke wake na watoto wake wawili kuungana naye nchini Uingereza. Kwa miaka hiyo yote, Pratik alifanya kazi kwa bidii, akiweka akiba na kupanga maisha bora kwa familia yake. Hatimaye, ndoto yao ilikuwa karibu kutimia.
Mnamo Jumatano asubuhi, familia hiyo ilipanda ndege ya Air India iliyokuwa ikielekea London kutoka Ahmedabad, wakijawa na furaha na matumaini. Kabla ya kuondoka, walichukua picha ya pamoja ndani ya ndege – picha hiyo, sasa imeenea duniani kote, ikiwakilisha furaha ya familia yenye matumaini mapya.
Lakini dakika chache baada ya ndege kupaa, tukio la kutisha lilitokea. Ndege hiyo ilianguka katika eneo la makaazi ya madaktari karibu na uwanja wa ndege, na kuleta maafa makubwa. Kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo, takriban watu 204 walithibitishwa kufariki dunia, lakini bado haijajulikana ni wangapi walikuwa ndani ya ndege na wangapi walikuwa ardhini wakati ajali hiyo ilipotokea.
Wakati jina la Pratik Joshi lilipoonekana miongoni mwa waliokuwa kwenye orodha ya abiria, hisia zikatawala mitandao ya kijamii. Picha ya familia hiyo ndogo – mume, mke na watoto wawili wadogo – ikisafiri kwa furaha kuelekea maisha mapya, iliwaliza watu wengi walioguswa na mkasa huo.
Taarifa kutoka kwa shirika la ndege Air India zilibainisha kuwa miongoni mwa abiria 242 waliokuwamo ndani ya ndege hiyo walikuwemo:
- 169 raia wa India
- 53 raia wa Uingereza
- 7 raia wa Ureno
- 1 raia wa Kanada
Wengi wa walioathirika walikuwa ni familia zinazohamia Uingereza kwa ajili ya maisha mapya, kama ya Pratik Joshi.
Katika taarifa rasmi, Tata Group, wamiliki wa Air India, walitangaza kuwa familia ya kila mtu aliyefariki itatunukiwa rupia milioni 1 (karibu pauni 86,000), pamoja na kulipia matibabu ya majeruhi na kurekebisha makaazi yaliyoathirika na ajali hiyo.
“Hakuna maneno yanayoweza kueleza maumivu tunayoyahisi kwa sasa,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Watu kutoka kila kona ya dunia wameonyesha mshikamano, wakituma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Hashtag kama #RememberPratik, #LifeIsShort, na #FamilyFirst zimekuwa zikisambaa mtandaoni, huku watu wakihimizana kupenda zaidi, kusamehe haraka, na kuishi kwa moyo mweupe, kwa sababu maisha hayawezi kutabirika.
Kwa wengi, kisa cha Pratik Joshi si tu kuhusu msiba wa ajali, bali ni kumbusho la maisha yenye thamani – maisha ya familia, ndoto, matumaini, na mapenzi yasiyo na mipaka.
#MANGWA
#AjaliYaNdege #AirIndiaCrash #PratikJoshi #PichaIliyogusaUlimwengu #MaishaNiMafupi #SalamuZaRambirambi #HabariZaDunia #IndiaToUK
