Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la SwissAid mwishoni mwa Mei 2025 imeibua tuhuma nzito dhidi ya mataifa ya Afrika Mashariki — Kenya, Rwanda, na Uganda — kwa kuhusika katika biashara ya kimataifa ya dhahabu ya magendo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan, Sudan Kusini na hata Ethiopia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mataifa haya, hususan Kenya, yamegeuka kuwa kitovu cha biashara hii haramu ya dhahabu kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Nairobi, mji mkuu wa Kenya, umetajwa kuwa na idadi kubwa ya viwanda vya kusafisha dhahabu (raffineries) vinavyodaiwa kutumika kama njia kuu ya usafirishaji wa dhahabu hiyo kuelekea Falme za Kiarabu (EAU), hasa Dubai, pamoja na India na Afrika Kusini.

“Sehemu kubwa ya dhahabu ya magendo kutoka DRC, Sudan Kusini, na Ethiopia hupitia Kenya kabla ya kufikishwa Dubai,” imeeleza ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizowekwa wazi, zaidi ya tani mbili za dhahabu hutoka DRC kila mwaka kwa njia ya magendo, ilhali katika mwaka wa 2023, serikali iliripoti kusafirisha kilo 672 pekee. Tofauti hii inaibua maswali kuhusu usimamizi wa rasilimali za nchi na ushiriki wa mataifa jirani katika uporaji wa utajiri wa Afrika.

SwissAid imeitaka Bunge la Kenya kuzingatia kwa kina mswada wa usimamizi wa dhahabu, ambao unalenga kuanzisha shirika rasmi la kudhibiti shughuli za usafishaji dhahabu nchini humo. Hata hivyo, shirika hilo linahofia kuwa sheria pekee haitoshi iwapo hakuna dhamira ya kweli ya kukomesha biashara hiyo haramu.

Kama ilivyofichuliwa, Kamlesh Pattni, mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu kutoka Kenya, aliorodheshwa na Marekani na Uingereza miongoni mwa watu 28 waliowekewa vikwazo vya kifedha mwaka jana kwa kuhusika na usafirishaji haramu wa dhahabu na utakatishaji wa fedha kupitia Zimbabwe.

Sakata hili linazidi kuibua maswali makubwa kuhusu:

  • Usalama wa rasilimali za bara la Afrika, hasa dhahabu kutoka DRC;
  • Uhusiano wa mataifa ya Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa ya dhahabu;
  • Na ufanisi wa vyombo vya kisheria katika kudhibiti usafirishaji haramu wa madini.

#MANGWA

#HabariZaAfrika #DhahabuYaMagendo #DRC #Kenya #Uganda #Rwanda #SwissAid #Uchunguzi #DuniaYaLeo

By mangwa