
Kolwezi, Juni 9, 2025 — Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, amewasili leo mchana katika mji wa Kolwezi, mji mkuu wa jimbo la Lualaba, kwa ajili ya ziara ya kikazi ya kufuatilia utekelezaji wa sera zake katika maeneo ya ndani ya nchi.
Akiwa ameambatana na Mkewe, Mama wa Taifa Denise Nyakeru Tshisekedi, Rais alipokelewa kwa shangwe kubwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kolwezi na Gavana wa Lualaba, Bi Fifi Masuka, pamoja na viongozi wa kisiasa na wa utawala kutoka ngazi za kitaifa na kikanda. Maelfu ya wananchi wa Kolwezi walijitokeza kumpokea kwa hamasa kubwa, wakishuhudia maendeleo yanayoendelea katika mji wao unaobadilika kwa kasi.
Katika ziara hii, Rais Tshisekedi atazindua na kutembelea miundombinu kadhaa mikubwa ya umma iliyojengwa kwa ufadhili wa fedha za serikali ya jimbo hilo tajiri kwa madini. Miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuzinduliwa ni pamoja na:
- Kijiji cha Mikutano (Village des Congrès) – kituo cha kimataifa cha mikutano,
- Jengo la abiria la uwanja mpya wa ndege wa kimataifa wa Kolwezi,
- Barabara za mzunguko wa mji (interchange),
- Barabara, madaraja na miundombinu ya usafirishaji,
- Hospitali na vituo vya afya.
Mojawapo ya matukio makuu katika ziara hii itakuwa ni mkutano wa mwaka wa 12 wa Wakuu wa Mikoa ya DRC (Magavana), utakaofanyika kuanzia Juni 10 hadi Juni 13, ukileta pamoja magavana 26 wa mikoa yote ya nchi.
Aidha, Rais Tshisekedi anatarajiwa kuongoza mkutano wa 47 wa Baraza la Mawaziri utakaofanyika huko huko Kolwezi, pamoja na kufanya mikutano na viongozi wa serikali na kuwasikiliza wawakilishi wa jamii za wenyeji kwa lengo la kupata maoni na malalamiko ya wananchi wa mashinani.
Ziara hii ya kikazi inalenga kufuatilia utekelezaji wa sera za serikali kuu katika maeneo ya ndani na kuhakikisha kuwa maagizo na mipango ya maendeleo inatekelezwa ipasavyo. Pia, inaleta fursa kwa Rais wa nchi kukutana ana kwa ana na wananchi wa maeneo ya mbali ili kusikiliza matatizo yao na kupanga njia mwafaka za kuyatatua.
✍🏽 Mwandishi: MANGWA



