#RDC 🇨🇩 | Vijana wa Mashariki Wasimulia Unyama wa M23: Watekwa, Wakafanywa Askari kwa Lazima
Katika ushuhuda wa kusikitisha uliotolewa na baadhi ya vijana waliotekwa na kundi la waasi la M23, imefichuka mateso makubwa wanayopitia vijana wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Vijana hao wamesema walitekwa kwa nguvu, wengine wakiwa raia wa kawaida na wengine wakiwa watoto wa askari wa FARDC, kisha wakalazimishwa kuwa wanajeshi wa M23.
Wameeleza kuwa wenzao wengi waliuawa kinyama na wanajeshi wa Kinyarwanda wanaomuunga mkono Corneille Nangaa, huku wao wakinusurika kwa bahati na kufanikiwa kutoroka.
Katika wito wa kusisimua, vijana hao wamewaomba wenzao waliobaki mikononi mwa M23 kujitenga na kundi hilo la kigaidi, ambalo linahusishwa na mauaji, ubakaji na utesaji wa raia wasio na hatia. “Ni wakati wa kujikomboa kutoka kwenye vita hii isiyo ya haki iliyoletwa na Rwanda,” wamesema kwa sauti ya uchungu.
Wamewataka vijana wote wa Kongo, popote walipo, kuinuka na kuungana katika harakati za kuikomboa nchi yao. “Ninyi mliobaki na M23, jitoeni kwa kundi hilo la kishetani. FARDC au WAZALENDO wako tayari kuwapokea na kuwaunganisha na jeshi la taifa ili kupigania uhuru wa kweli wa Kongo,” waliongeza kwa matumaini.
Wito huu unakuja wakati taifa likikabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama, huku maelfu ya raia wakipoteza maisha yao na wengine wengi kuachwa bila makazi kutokana na uvamizi wa mara kwa mara wa M23 na washirika wake.
