
Ituri yaomboleza: CENCO yalaani mauaji ya waumini Kanisani Komanda
Mkoa wa #Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umezama katika huzuni kubwa kufuatia mauaji ya kutisha yaliyotekelezwa usiku wa kuamkia Julai 27, 2025, huko Komanda, ndani ya jimbo la Bunia. Wakati wa tukio hilo la kusikitisha, wanaume, wanawake na watoto waliokuwa wakijumuika katika sala ndani ya jumba la parokia waliuawa kinyama, hali iliyotikisa jamii nzima ya wakristo na raia kwa ujumla.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa Julai 28, 2025, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kongo (#CENCO) limeshutumu vikali tukio hilo, likilitaja kuwa ni tendo la “kishetani” na kuonyesha masikitiko yake kwa familia za wahanga, majeruhi na Askofu #Dieudonné Uringi wa jimbo la Bunia. Baraza hilo limeahidi mshikamano wa kiroho na wa upendo kwa wote walioguswa na tukio hilo la kusikitisha.
Tukio hili linajiri siku chache tu baada ya kufanyika kwa kitendo cha kufuru dhidi ya Kanisa la Lopa, pia ndani ya Ituri – jambo linaloonesha kuzidi kwa ukosefu wa usalama hata katika maeneo ya ibada, licha ya kuwepo kwa majeshi ya FARDC, UPDF ya Uganda, na walinda amani wa MONUSCO, katika eneo hilo lililo katika hali ya hatari kwa miaka kadhaa sasa.
CENCO imezitaka mamlaka za kitaifa kuchukua hatua za haraka na kufanya uchunguzi wa kina, huru na wa uwazi kuhusu mashambulizi haya, huku ikisisitiza kuwa watu wa Kongo wanastahili haki, ukweli, na zaidi ya yote – amani ya kweli.
Baraza hilo pia limewataka waumini kutoogopa, bali waendelee kuomba kwa ajili ya roho za marehemu na kupigania mustakabali wa maisha ya pamoja ya amani, wakijikabidhi kwa imani na tumaini.
Katika hitimisho la tamko lake, #CENCO imetoa mwito wa maombi kwa maombezi ya Bikira Maria, Mfariji wa walio na huzuni, ili amani irudi haraka iwezekanavyo katika taifa la Kongo.
🕊 “Walikuja kuomba, wakaishia kuuawa. Tuwaombee. Tuamke.”
Mama Mwiza: Sauti ya Uponyaji Mashariki mwa Congo
Uganda yatishia kuichukua Kisangani kabla ya mwisho wa 2025
Koloneli Daniel Mukalay Aachiwa Huru Baada ya Miaka 14, Familia ya Chebeya Yalia kwa Uchungu
Fayulu: “Nilinyang’anywa ushindi, lakini sikubeba silaha”
