Patrick Muyaya kwa Vijana wa UNIKIN: “Rwanda si mfano wa kuigwa, ni mnyonyaji”

Katika mkutano mkubwa wa vijana uliofanyika Jumatano, Julai 25, 2025, kwenye Chuo Kikuu cha Kinshasa (UNIKIN), Waziri wa Mawasiliano na Vyombo vya Habari, Patrick Muyaya Katembwe, alitoa hotuba kali yenye ujumbe mzito kuhusu amani, uzalendo, na mustakabali wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akiwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa mjadala uliokuwa na kauli mbiu “Katika moyo wa mchakato wa kupatikana kwa amani ya DRC – Kuelewa ili kutenda,” Muyaya aliwahimiza vijana kumiliki simulizi la taifa lao na kutokubali kupotoshwa na taswira zinazojengwa na mataifa jirani, hasa Rwanda.

“Rwanda si mfano wa kuigwa kama wengine wanavyodai, ni mnyonyaji (prédateur),” alisema bila kuuma maneno, akishangiliwa na mamia ya wanafunzi waliokuwa ukumbini.

Waziri huyo aliipongeza diplomasi ya Rais Félix Tshisekedi na kufichua kuwa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Gasabo nchini Rwanda tayari kimeshapigwa marufuku na Umoja wa Ulaya – jambo linaloashiria mafanikio ya mikakati ya kidiplomasia ya DRC kimataifa.

Aidha, Muyaya alisisitiza nafasi ya DRC kama nchi ya kipekee barani Afrika:

“Tuna majirani tisa, lakini ukichunguza kwa makini, wengi wao wanatutegemea – iwe kiuchumi, kijeshi au kimkakati. Ni sisi tunapaswa kurejesha heshima yetu kama taifa kuu la ukanda huu.”

Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa changamoto kubwa ya DRC si tu mashambulizi kutoka nje, bali ni urejeshaji wa udhibiti wa simulizi la kitaifa, ambapo alihimiza vijana kusoma historia, kujifunza utajiri wa nchi yao, na kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa amani ya kudumu.

Mkutano huu ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya kuelimisha vijana kuhusu utambulisho wa kitaifa, umiliki wa rasilimali, na umuhimu wa kuwa mstari wa mbele katika ulinzi wa mamlaka na heshima ya nchi.

mecamediaafrica.com

Ituri: Mke wa kiongozi wa kijiji na mtoto wajeruhiwa kwa bomu