
🇨🇩 Waziri wa Ulinzi Guy Kabombo Afanya Ziara Muhimu Katika Vituo vya Kijeshi vya FARDC
Waziri Mkuu Msaidizi na Waziri wa Ulinzi na Mashujaa wa Taifa, Guy Kabombo Muadiamvita, amefanya ziara ya ukaguzi katika Kituo cha Juu cha Mafunzo ya Kijeshi (CSM) – makao ya shule mbalimbali za kijeshi za Jeshi la Wananchi wa Congo (FARDC) mjini Kinshasa.
Katika ziara hiyo, Guy Kabombo alipokelewa na Luteni Jenerali Obed Rwibasira Ruyumbu, Kamanda Mkuu wa shule hizo, na kupatiwa taarifa ya kina na maafisa waandamizi wakiwemo Kanali Mamina Dieudonné na Jenerali Meja Monique Ngomo, kuhusu changamoto zinazoikumba sekta ya mafunzo ya kijeshi nchini. Miongoni mwa matatizo yaliyoainishwa ni:
- Uwezo mdogo wa kupokea wanafunzi
- Majengo chakavu ya shule ya awali na nyumba za kijamii
- Upungufu wa vifaa vya kufundishia na motisha kwa walimu
Kamanda wa shule alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa shule za kadeti (cadet schools) ili kukuza uzalendo kwa watoto wa Congo.
Waziri Kabombo aliahidi kushughulikia changamoto ndogo mara moja, na zile za msingi kuzifikisha kwa Kamanda Mkuu wa FARDC, Rais wa Jamhuri.
Baada ya CSM, Waziri Kabombo alitembelea Ofisi ya Ukaguzi Mkuu wa FARDC ambako alielezwa kuhusu kazi ya ukaguzi wa ndani na udhibiti wa miundo ya kijeshi. Hapa, aliwataka maafisa kutekeleza kazi kwa ukali na uadilifu, pasipo kuingiliwa kisiasa.
Ziara hiyo pia ilimfikisha kwenye Makao Makuu ya Idara ya Ujasusi wa Kijeshi, ambako alipokelewa na Jenerali Meja Jean Roger Makombo Mwinaminayi, na kupewa taarifa kuhusu namna huduma hiyo inavyofanya kazi katika maeneo yote ya ulinzi nchini. Waziri Kabombo alieleza dhamira ya kuimarisha huduma hiyo muhimu, hasa ikizingatiwa kuwa ilikuwa ziara ya kwanza ya waziri wa ulinzi kwa zaidi ya miaka 15.
Ziara hizi zinafanyika katika kipindi kigumu cha vita ya uvamizi kutoka Rwanda kupitia AFC/M23, ambapo FARDC inahitajika kuimarishwa kwa haraka.
Ahadi za Waasi DRC Zazidi Kuvunjika
Kambi ya CHAN ya Congo Yaahirishwa Kwa Ukata
Doha Yafungua Mlango wa Amani DRC na M23
