
KUTOWEKA KWA JACQUES KYABULA: DGM YAANZA UCHUNGUZI WA KINA KUJUA ALIKO
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imechukua hatua kali kufuatia kutoweka kwa aliyekuwa Gavana wa mkoa wa Haut-Katanga, Jacques Kyabula Katwe. Tarehe 18 Julai 2025, Mkurugenzi wa Mkoa wa Idara ya Uhamiaji (DGM) katika Haut-Katanga alitoa amri rasmi kwa maafisa wake wote kuimarisha ulinzi na kufungua uchunguzi wa kina juu ya mahali alipo mwanasiasa huyo.
Katika waraka ulioandikwa rasmi, maafisa wa DGM wametakiwa kufanya uchunguzi wa ndani na wa kimataifa ili kubaini iwapo Kyabula bado yupo katika ardhi ya taifa au amesafiri kwa siri nje ya nchi, akiepuka mifumo rasmi ya uhamiaji. Waraka huo umetilia mkazo kuwa taarifa yoyote ya kutiliwa shaka lazima itolewe mara moja.
Hatua hii inakuja baada ya kutoweka kwa Kyabula kunakotajwa kuwa kwa muda mrefu na kusababisha maswali mengi, hasa baada ya kuitwa Kinshasa kutokana na matamshi yake yenye utata kuhusu Rais wa zamani Joseph Kabila na mwanasiasa Corneille Nangaa. Taarifa zinasema huenda alikuwa anatarajiwa kufanyiwa mahojiano rasmi ya kisiasa au kisheria.
Hadi sasa, Kyabula wala watu wake wa karibu hawajatoa taarifa yoyote kwa umma juu ya mahali alipo. Hii imezidisha hofu kwamba huenda amekimbia nchi ama kwa sababu za kiusalama au kuepuka mchakato wa kisheria unaoweza kumkabili.
Idara ya Uhamiaji imesisitiza kuwa itachukua hatua zote zinazostahili kuhakikisha kuwa jambo hili linafanyiwa uchunguzi wa kina na ukweli kufahamika, huku mamlaka za usalama zikiendelea kufuatilia kila taarifa muhimu.
DRC na M23 Wafikia Makubaliano ya Amani Doha
Kinshasa Yaitaka Uganda Kutoa Maelezo kwa Kufungua Mpaka na M23
Imeandikwa na MANGWA
