
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, amejitokeza kwa maneno mazito dhidi ya serikali, akisema hawezi kuwa sehemu ya mfumo usiojali misingi ya haki, sheria na katiba ya nchi. Katika hotuba yake kupitia Facebook, Polepole amethibitisha kujiuzulu nafasi yake, huku akifichua kuwa dada yake ametekwa na kuumizwa na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwake kwa kuruka ukuta.
Katika taarifa aliyoiweka Instagram, Polepole alisema tukio hilo lilifanyika usiku wa kuamkia leo, na ni jaribio la kumtisha kabla ya hotuba yake ya leo. Ameapa kutonyamazishwa, hata kama familia yake yote itatekwa.
Kamanda wa kanda maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Katika hotuba hiyo, Polepole alikosoa vikali namna Rais Samia Suluhu Hassan na Dkt. Emmanuel Nchimbi walivyochaguliwa kugombea nafasi ya Urais na Makamu wake kupitia CCM, akidai kuwa mchakato huo ulikiuka utaratibu wa chama.
BBC bado inafuatilia kupata kauli ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu tuhuma hizo.
Licha ya kuwa mtetezi sugu wa CCM na marehemu Rais John Magufuli, Polepole amewahi pia kulaumu chama hicho kwa kuwa na “watu wahuni” wanaotumia uchawi na fitina kuwang’oa wanachama waadilifu.
Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwenye mustakabali wake wa kisiasa baada ya kujiuzulu balozi na kuanzisha ukosoaji waziwazi dhidi ya uongozi wa sasa.
