RAIS PAUL BIYA AWEKA BAYANA: ATAGAZA KUGOMBEA URAIS TENA KWA MARA YA NANE AKIWA NA MIAKA 92

Yaonekana hakuna mwisho kwa uongozi wake, huku sauti za upinzani na wasiwasi wa kimataifa zikipanda

YAOUNDE, CAMEROON – Katika tangazo lililowashangaza wengi lakini pia kuwahuzunisha wengine, Rais mkongwe zaidi duniani, Paul Biya mwenye umri wa miaka 92, ametangaza rasmi nia yake ya kugombea tena urais wa Cameroon katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 12, 2025.

Tangazo hilo, lililotolewa kupitia mitandao ya kijamii Ijumaa hii, linaashiria azma ya Biya ya kuendelea kuongoza taifa hilo la Afrika ya Kati kwa muhula wa nane, licha ya utawala wake wa takriban miaka 43 kukabiliwa na shutuma nzito za ufisadi, udikteta, ukosefu wa usawa wa maendeleo, na kukandamiza upinzani.

“Mimi ni mgombea wa uchaguzi wa urais wa Oktoba 12,” aliandika Biya kwa ujasiri. “Uamuzi wangu umetokana na simu nyingi kutoka mikoa yote kumi ya nchi yetu na kutoka kwa ndugu zetu walioko ughaibuni.”

Biya pia alisisitiza kuwa bado ana dhamira ya kulihudumia taifa kwa bidii, licha ya hali ya uzee wake na changamoto zinazoendelea kumkabili, ikiwemo mizozo ya ndani ya silaha, ukosefu wa ajira kwa vijana, na migogoro ya kisiasa inayozidi kushamiri.

Talaka ya kisiasa na ufa wa kihistoria

Tangazo lake linakuja wakati ambapo ushawishi wake unaonekana kuyumba, hasa baada ya kuvunjika kwa ushirikiano na baadhi ya washirika wake wa karibu kutoka mikoa ya kaskazini — ngome muhimu ya kura zake katika chaguzi zilizopita. Hii imezua maswali kuhusu uwezo wake wa kushinda kwa urahisi kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Pia, wito wa kumtaka ajiondoe madarakani umeongezeka kutoka kwa makundi ya kiraia, vijana, na hata baadhi ya viongozi wa kimataifa, wakimtaka kutoa nafasi kwa kizazi kipya chenye maono mapya kwa Cameroon.

Kama atashinda… karibu na miaka 100 akiwa madarakani

Iwapo Paul Biya atashinda uchaguzi wa Oktoba, atakuwa anamaliza muhula mwingine wa miaka saba, na hivyo kuwa karibu kufikisha umri wa miaka 100 akiwa bado ni Rais. Hii itamweka katika orodha ya viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi katika historia ya dunia ya kisasa.

Kwa sasa, wadadisi wa siasa na raia wa Cameroon wanasubiri kwa hamu kuona kama wagombea wa upinzani wataweza kusimama kidete dhidi ya mtindo wa uongozi wa muda mrefu wa Biya, na kama kutakuwa na mazingira ya uchaguzi wa haki, huru, na wa kidemokrasia.

Imeandikwa na MANGWA