Kukamatwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC), Jenerali Christian Tshiwewe, kumefumua mtikisiko mpya katika duru za kisiasa na kijeshi za nchi hiyo, baada ya mbunge Eliezer Ntambwe kutoa maelezo ya kushangaza kuhusu tukio hilo.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo kutoka muungano wa Union Sacrée, Tshiwewe hakukamatwa kwa sababu ya jaribio la mapinduzi kama ilivyodaiwa awali, bali kwa sababu za kisiasa na binafsi. Katika maelezo yake, Ntambwe alidai kuwa Tshiwewe alinukuliwa akiwa amemweleza Rais wa zamani Joseph Kabila kwamba yeye ndiye “anayemdhibiti Rais wa sasa Félix Tshisekedi” na hata kudai kuwa “Tshisekedi atatolewa hivi karibuni.”

Kauli hizi, endapo zitathibitishwa, zinaibua maswali mazito kuhusu uhusiano wa ndani ya jeshi na siasa za DRC. Zinaonyesha jinsi mvutano na ukosefu wa uaminifu vinavyoenea miongoni mwa vigogo wa kijeshi na kisiasa.

Mbunge Ntambwe pia alikanusha taarifa kwamba Tshiwewe amefungwa katika gereza la kijeshi la Ndolo, akisema kuwa yuko katika eneo lisilojulikana kwa sasa. Hii imezidi kuchochea hali ya sintofahamu kuhusu hali ya kweli ya tukio hilo.

Katika juhudi za kuweka muktadha wa matukio, Ntambwe alikumbusha kuwa ni Rais Tshisekedi aliyempa Tshiwewe cheo cha Jenerali wa Nyota Nne – heshima ambayo hakuwahi kupewa chini ya utawala wa Kabila licha ya wote kuwa kutoka mkoa wa Katanga. Alieleza kuwa Tshisekedi ameonyesha ukarimu mkubwa kwa watu wa Katanga, akiuliza kwa mshangao: “Ni kitu gani Rais hajawapa watu wa Katanga?”

Taarifa hizi zimezua taharuki kubwa nchini, huku wananchi wakitaka ukweli kamili ujulikane. Serikali bado haijatoa tamko rasmi juu ya madai hayo mapya, jambo linaloacha ombwe la maelezo kwa umma. Hali hii imefanya waangalizi wa siasa nchini kutoa wito kwa uchunguzi huru na wa wazi ili kuweka wazi ukweli wote wa nyuma ya pazia.

Tukio hili linazidi kuonesha ugumu wa Rais Tshisekedi katika kusawazisha nguvu za kisiasa na kijeshi ndani ya taifa ambalo bado linatafuta uthabiti wa kitaifa.

🖊 Muandishi: MANGWA