Watu 9 wa Familia ya Rais Tshisekedi Washitakiwa Brussels kwa Wizi wa Madini

Brussels, Ubelgiji – Watu tisa wa familia ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, akiwemo mke wake Denise Nyakeru Tshisekedi, wamefunguliwa mashitaka mjini Brussels wakituhumiwa kwa wizi wa madini, rushwa, na ushiriki kwenye shughuli za kihalifu zinazohusiana na migodi katika majimbo ya Lualaba na Haut-Katanga.

Kwa mujibu wa vyanzo vya mahakama, mashtaka hayo yaliwasilishwa na mawakili kwa niaba ya mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali kutoka Katanga, pamoja na maafisa wa zamani wa kampuni ya serikali ya madini, Gécamines.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na watoto wa Rais, kaka zake, na shemeji wa familia, ambao wote wanadaiwa kuwa na uraia wa Ubelgiji – jambo linalofanya kesi hiyo kuendeshwa chini ya sheria za Ubelgiji.

Kesi hiyo inalenga kufichua madai ya ufisadi mkubwa na kutumia mamlaka kwa manufaa binafsi, ambapo familia hiyo inadaiwa kufaidika kifedha kupitia upendeleo katika utoaji wa leseni za madini na usimamizi wa rasilimali za taifa.

Mashirika ya kiraia yaliyofungua kesi hiyo yamesema kuwa hatua hii inalenga kulinda utajiri wa taifa la Kongo dhidi ya uporaji wa kifamilia, na kuitaka mahakama ya Brussels kuhakikisha haki inatendeka.

Mpaka sasa, hakujatolewa tamko rasmi kutoka kwa Ikulu ya Rais wa Congo wala kutoka kwa mawakili wa washitakiwa. Hata hivyo, hatua hii ya kisheria imezua mjadala mkubwa kuhusu uwajibikaji wa familia ya viongozi wa juu serikalini, hasa kwa wale wanaoshikilia uraia wa nchi za nje.

🖋 Mwandishi: MANGWA