RDC: M23 Inayotegemezwa na Rwanda Yadai Udhibiti Kamili wa Kivu Kaskazini na Kusini kwa Miaka 8!

Katika mazungumzo yanayoendelea mjini Doha, Qatar, kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC) na Rwanda, chanzo cha karibu na ujumbe wa Congo kimefichua kwa Shirika la Habari la Congo (ACP) kuwa kundi la waasi la M23/AFC, linaloungwa mkono na Kigali, linataka kudhibiti kwa ukamilifu mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini kwa kipindi cha miaka minane.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, madai hayo yanahusu usimamizi kamili wa nyanja zote za kiutawala, usalama, uchumi, na siasa katika maeneo hayo mawili muhimu ya mashariki mwa Congo. Hatua hiyo inatambuliwa na wachambuzi kama jaribio la “uvamizi wa kiutawala” uliojificha chini ya kivuli cha mazungumzo ya amani.

“Madai makuu ya M23-AFC katika mazungumzo ya Doha ni kupata mamlaka ya pekee ya kuongoza mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kwa kipindi cha miaka minane,” chanzo hicho kilieleza.

Madai haya yanazidisha hofu ya wacongo wengi ambao tayari walikuwa wakishuku dhamira halisi ya Rwanda kupitia usaidizi wake wa kijeshi na kisiasa kwa M23. Wakati ambapo dunia inatarajia suluhu ya amani, madai haya yanaonekana kuyumbisha misingi ya mamlaka ya kitaifa ya DRC.

Ni wazi sasa kuwa mazungumzo ya Doha hayahusu tena tu usitishaji wa mapigano, bali pia mwelekeo wa baadaye wa maeneo ya mashariki ya Congo – na mustakabali wa watu wake.

muandishi ni MANGWA

Chanzo: Agence Congolaise de Presse (ACP)👉 https://www.acp.cd